Wanafunzi tisa wamethibitishwa kufariki katika eneo la Greater Accra nchini Ghana Jumatano baada ya boti iliyokuwa ikiwapeleka shuleni kupinduka.
Watoto wa shule walisemekana kusafiri kutoka Faana hadi Kelee katika Manispaa ya Ga Kusini ya Mkoa wa Accra Mkuu.
Walikuwa na umri wa kati ya miaka 8 na 15, 3news.com iliripoti Alhamisi.
Miili ya watoto wanane iliyopatikana awali ilitumwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Korle Teaching.
Mwili wa mtoto wa 9 uliokotwa Alhamisi asubuhi baada ya msako mkali wa vijana katika jamii.
Mkurugenzi wa Manispaa wa Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga (NADMO), Christian Afiadenyo, aliambia vyombo vya habari vya ndani kuwa wanafunzi watatu walinusurika kwenye janga hilo.
Alisema mvulana mmoja kati ya wanafunzi alikuwa akiendesha boti kabla ya tukio hilo kutokea ingawa hana uhakika kuhusu habari hii.
Bw Afiadenyo alisema huenda mvulana huyo alikuwa mmoja wa watu watatu walionusurika.
Inasemekana mji huo ulitupwa katika hali ya maombolezo tangu kutokea kwa tukio hilo.