Kampuni ya Lake Group imeanza utekelezaji wa vitendo wa mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabiachi kwa kujenga matanki ya kuhifadhi na kusambaza gesi itakayookoa matumizi ya nishati ya mkaa na kuni kupikia.
Matanki hayo yenye uwezo wa kuhifadhi tani zaidi 100,000 yamejengwa katika bandari ya Tanga jijini hapa ikiwa pia ni maandalizi ya kuwawekea mazingira rafiki wageni wanaotarajia kuwekeza mkoani Tanga miradi mbalimbali.
Mwenyekiti wa Lake Group,Ally Edha Awadh alitoa taarifa hiyo wakati wa uzinduzi wa ghala la kisasa lenye matanki ya kuhifadhia gesi yaliyopo Jijini hapa.
Alisema katika kutekeleza kwa vitendo kampeni ya Kitaifa na kimataifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na kuhakikisha misitu haiteketezwi kwa ajili ya matumizi ya.kuni na mkaa Lake gas imedhamiria kuwekeza katika kupeleka nishati hiyo kwa bei nafuu.
“Tumeanza kujenga matanki haya ya kuhifdhia gesi itakayouzwa kwa wananchi ikiwa ni nishati mbadala wa kuni na mkaa ambao unatokana na vunaji wa kasi wa mkaa na kuni” alisema Awadhi.
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Absa,Obed Laiser alisema baada kutokana na ukweli kuwa nishati ya gesi inaweza kutumika kama mbadala wa matumizi ya kuni na mkaa,benki hiyo imeamua kuiunga mkono Lake Group kwa kuipa mkopo uliowezesha kujengwa matanki ya gesi katika eneo la chumvini Jijini Tanga.
“Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni kampeni ya kitaifa na kimataifa kwa maana hiyo tunaunga mkono uwekezaji wa nishati mbadala ili misitu isiendelee kuteketezwa kwa sababu madhara yake ni pamoja na kukosekana kwa mvua na kuongezeka hewaukaa Diniani” alisema Laiser.
Feuzi Bano wa Mkata Wilayani Handeni alisema pamoja na kwamba matumizi ya gesi yameanza kushamiri kwa wakazi wa mijini lakini inahitajika kufanyika kampeni kubwa ya kuwahamasisha wakazi wa vijijini.
“Wananchi wa vijiini bado hawajahamasika kutumia gesi kwa sababu wapo katika mazingira yanayozunguka miti kwa hivyo uvunaji wa misitu unazidi kuongezeka ni vyema ikatumika mbinu kubwa kuhakikisha kampeni ya kuhifadhi mazingira inaongezewa nguvu” alisema Bano.