Wajumbe wa Chama cha National Democratic Congress (NDC) walipiga kura katika kura za mchujo mwishoni mwa juma kumchagua mgombeaji wa kura zote mbili za urais na ubunge ambapo Rais huyo wa zamani alipendekezwa na wachambuzi wengi wa kisiasa kushinda mchujo kutokana na uzoefu na ushawishi wake katika chama cha upinzani.
Mahama alitangazwa mshindi kwa wingi baada ya kupata asilimia 98.9 ya kura huku mpinzani wake, meya wa zamani wa Kumasi Kojo Bonsu akipata asilimia 1.1.
“Amejaribiwa na kujaribiwa na anakuja na uzoefu mkubwa,” Kwame Asah-Asante, mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Ghana alisema.
Imani hii kwa Mahama iliungwa mkono na wengi wa wajumbe zaidi ya 355,000 wa chama cha NDC waliokusanyika katika vituo 401 vya kupigia kura kote nchini mwishoni mwa juma kwa ajili ya upigaji kura.
“Ninaamini kama NDC ikichukua madaraka, mambo mengi ambayo sisi Waghana tunataka, NDC inaweza kuja kutufanyia. Kwa mfano, kutunza watoto wetu. Upande wa pili ulituahidi mengi ambayo hawakuweza kutimiza,” alisema. Alisema mfanyabiashara Kafur Addo.
Anasema anaamini kuwa NDC ikiingia madarakani, chama hicho kitatimiza ahadi walizoahidi.
Uchaguzi wa mchujo unakuja wakati Ghana inafanya mazungumzo na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuhusu uokoaji wa dola bilioni 3 ili kusaidia kukabiliana na mzozo wa kiuchumi, na huku ikikabiliwa na tishio la wanajihadi linaloongezeka kutokana na mzozo katika nchi jirani ya Burkina Faso.
Chama tawala cha Rais aliye madarakani Nana Akufo-Addo kitafanya uchaguzi wake wa mchujo mwezi Novemba, na uchaguzi wa urais umepangwa kufanyika tarehe 7 Desemba 2024.
Rais huyo wa zamani wa Ghana aliongoza nchi hiyo kuanzia Julai 24 2012 hadi Januari 7, 2017 kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wakati huo John Attah Mills.
Aliwahi pia kuwa makamu wa rais kuanzia Januari 2009 hadi Julai 2012.
Mahama anatazamiwa kulitumia zaidi suala la hali mbaya ya uchumi inayoikabili nchi hiyo ya Afrika Magharibi katika kampeni za uchaguzi wa rais.
Ghana, ambayo ni muuzaji mkubwa wa kakao na dhahabu nje ya nchi, imeshindwa kulipa madeni yake ya nje na iko katika mazungumzo na IMF kwa ajili ya kupatiwa mkopo wa dola bilioni 3 ili kuimarisha uchumi wake.
Chama tawala cha New Patriotic Party kitafanya mchujo wake wa wagombea mwezi Novemba 2023 huku uchaguzi wa rais ukipangwa kufanyika Desemba 7 mwaka ujao.