Chelsea iko mbioni kuajiri meneja mpya wa kikosi cha kwanza baada ya kumfukuza Graham Potter.
The Blues kwa sasa wanaongozwa na Frank Lampard ambaye aliteuliwa kwa muda klabu hiyo huku jukumu lake kama meneja wa muda litakamilika mwishoni mwa msimu huu.
Chelsea wanakaribia kufikia makubaliano na Mauricio Pochettino wakitafuta mbadala wa muda mrefu wa Graham Potter. Mazungumzo yanaendelea kati ya The Blues na meneja wa zamani wa Tottenham na Paris St Germain, 51, lakini makubaliano rasmi bado hayajakamilika.
Tangu Potter aondoke bila kutarajiwa mwezi uliopita, Frank Lampard amekuwa akihudumu kama kocha wa muda hata hivyo, timu hiyo imefanikiwa kupata ushindi mmoja pekee katika mechi nane chini ya uongozi wake katika kipindi chake cha pili kwenye usukani. Mkimbio huu wa kusikitisha uliishia kwa sare ya 2-2 dhidi ya Nottingham Forest katika uwanja wa Stamford Bridge wikendi.
Huku mechi tatu za Premier League zikiwa zimesalia dhidi ya Manchester City, Manchester United, na Newcastle, Chelsea wanalenga kuwa na meneja wao mpya mara tu kampeni za sasa zitakapokamilika. Licha ya uwekezaji mkubwa kwenye kikosi cha wachezaji, The Blues wamevumilia msimu wa kukatisha tamaa, wakiwa wamekaa katika nafasi ya 11 na kushinda mara 11 pekee katika mechi 35 za ligi.