Katika kuendeleza soko la filamu nchini waandaaji na waigizaji wa filamu wametakiwa kuzalisha kazi bora za sanaa zenye ushindani ili ziweze kushindanishwa na kuona kazi bora ambapo wametaja kuwa ni kuendeleza jitihana za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sanaa.
Hayo yametajwa na Mkurugenzi wa idara ya maendeleo ya filamu kutoka bodi ya filamu Tanzania Emmanuel Ndumukwa akiwa mkoani Morogoro wakati wa ufunguzi wa mchakato wa awali wa maandalizi ya tuzo kwa waandaaji na waigizaji wa filamu ndani ya mkoa wa Morogoro (Morogoro Film Festival Awards) na amewataka waandaaji na waigizaji wa filamu kupeleka kazi zao kwenye jukwaa hilo ili ziweze kushindanishwa.
Pia ameitaka mikoa mingine nchini kuhakikisha inaendelea kuandaa matamasha hayo ili yaweze kuwasaidia waandaaji na waigizaji wa kazi za sanaa kujipambanua zaidi katika jamii lakini pia kuwawekea ushindani ambao utawasaidia kuendelea kuzalisha filamu zenye ubora na viwango vinavyohitajika kwenye soko la filamu ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha waigizaji mkoa wa Morogoro Ramadhan Khamis amesema kuwa lengo la kuandaa jukwaa hilo la filamu ni kuwapa heshima wadau wa filamu na kuongeza ushindani katika soko huku mmoja ya walimu wa sanaa akawataka waigizaji na watayarishaji wa kazi za sanaa kuigiza na kuishi kiuhalisia kulingana na maadili ya jamii.
Tuzo hizo zimezoandaliwa na chama cha filamu mkoa wa Morogoro zinatarajia kutolewa mwishoni mwa mwezi wa tisa huku zaidi ya wanasanaa mia mbili wanatarajia kushindanisha kazi zao.