Zelenskyy alikanusha madai ya Russia kwamba ilikuwa imeutwaa mji wa Bakhmut. Siku ya Jumamosi, Russia ilisema imeuteka mji huo uliokumbwa na msukosuko baada ya vita vilivyodumu kwa miezi tisa huko, ambavyo vinatajwa kama vilivyosababisha umwagikaji wa damu zaidi, tangu vita vya pili vya dunia.
Rais huyo wa Ukraine alisema mwishoni mwa mkutano wa viongozi wa mataifa tajiri zaidi duniani G-7, mjini Hiroshima, Japan, kwamba Russia haikuwa imeuteka kabisa mji wa Bakhmut kama alivyodai Rais Vladmir Putin.
Usiku wa Mei 20 kuamkia 21, Wizara ya Ulinzi ya Urusi na Vladimir Putin mwenyewe walidai kwamba vikosi vya Urusi, vinavyohusishwa na kundi la wanamgambo la Wagner, vinashikilia udhibiti kamili wa mji wa Bakhmut huko Donbass.
Katika siku za hivi karibuni, jeshi la Ukraine lilidhibiti tu vitalu vya majengo magharibi mwa Bakhmut, labda 5% ya eneo la wilaya, lakini vikosi vya Urusi vimeongeza kasi ya operesheni katika saa 48 zilizopita, hadi kufikia usiku wa Ijumaa kuamkia Jumamosi, askari wa Ukraine walirekodi video kwenye simu zao, wakitangaza kuanguka kwa jiji hilo, anasema mwandishi wetu wa Kiev, Stéphane Siohan.
Rais huyo alionya kwamba ikiwa ulimwengu hautaungana dhidi ya mvamizi wa Russia, itakuwa “suala la muda tu kabla ya wahalifu wengine kutaka kuanzisha vita kama hivyo,” na kuongeza kwamba, alikuwa mjini Hiroshima ili ulimwengu usikie wito wa Ukraine wa kuungana pamoja kutoka huko.
Mapigano ya miezi tisa ya Bakhmut, yameharibu mji huo wa mashariki mwa Ukraine ambao umekuwepo kwa miaka 400 na kuua darzeni za maelfu ya watu, huku Ukraine ikitumia mkakati ulionuiwa kulichosha jeshi la Russia, Shirika la habari la AP limeripoti.
Ukungu uliosababishwa na mashambulizi uliifanya vigumu kuthibitisha hali ilivyokuwa Jumapili, katika vita virefu zaidi tangu uvamizi wa Russia kuanza nchini Ukraine, huku wizara ya ulinzi ya Russia ikiripoti kwamba kikosi cha kibinafsi cha Wagner, kikisaidiwa na wanajeshi wa Russia, kilikuwa kimeuteka mji huo.
Licha ya yote hayo, mji huo mdogo, kwa muda mrefu umekuwa ni wa kuonyesha taswira ya kiishara zaidi kuliko thamani yake ya kimkakati kwa pande zote mbili, kwa mujibu wa wachambuzi.
Kigezo cha kweli zaidi, cha mafanikio kwa vikosi vya Ukraine, kimekuwa uwezo wa wanajeshi wake kuvizuia vikosi vya Russia.