Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi atazuru China wiki ijayo huku mataifa hayo mawili yakitarajia kuhitimisha mazungumzo ya upya wa mkataba wa dola bilioni 6.2 wa madini kwa ajili ya miundombinu, watu wenye ufahamu wa moja kwa moja wa safari hiyo walisema.
Ziara hiyo ilitangazwa na wizara ya mambo ya nje ya China siku ya Jumatatu na mkutano utafungua njia kwa nchi hizo mbili kufanya marekebisho rasmi na kusaini mkataba na wawekazaji kutoka China wa dola bilioni 6 kwa miundombinu kwa ajili ya madini.
Tshisekedi aliagiza serikali yake wakati wa kikao cha Baraza la Mawaziri cha tarehe 19 mwezi Mei kuendelea na mazungumzo kuhusu makubaliano ya kibiashara na wenzao wa China baada ya serikali ya DRC na wadau wengine “kuimarisha msimamo wao,” taarifa ya serikali ya DRC ilisema.
Aliwafahamisha wajumbe wa Baraza la Mawaziri kwamba kikosi kazi kinachoshughulikia mpango huo kimewasilisha mahitimisho yake, na kuwezesha majadiliano na washirika wa China kuanza katika siku zijazo.
Wakati wa ziara hiyo nchini China, wakuu hao wawili wa nchi watafanya mazungumzo na kuhudhuria hafla ya utiaji saini hati za ushirikiano, wizara ya mambo ya nje ya China ilisema.
“Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni nchi muhimu barani Afrika, na urafiki kati ya China na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ina historia ndefu,” msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning alisema katika mkutano wa mara kwa mara na waandishi wa habari.