MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga, Rajab Abdulhaman Abdallah, amesema wenyeviti wa vijiji na vitongoji waliotoa ardhi kinyume cha taratibu na kusababisha migogoro ya ardhi, hawatakuwa na nafasi ya kurudishwa majina yao katika Uchaguzi wa serikali za mitaa hapo mwakani endapo watagombea tena.
Akizungumza katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku kumi, kushukuru na kuhamasisha Utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025, alisema kuwa wapo badhi ya wenyeviti kwa kushirikiana na Serikali yake ya kijiji, wamesababisha migogoro ya ardhi katika maeneo yao kwasababu zao binafsi.
Alisema migogoro hiyo imesababishwa kutokana na uuzaji holela unaofanywa na viongozi hao bila kuzingatia taratibu zinazotakiwa kufuatwa kwa mwekezaji anayetakiwa kumiliki ardhi katika ngazi za vijiji.
Alisema Viongozi hao wameuza maeneo ya ardhi kiasi kikubwa na zaidi ya Ekari 200 katika kijiji wakitumia kuandika mutasari iliyokuwa na sahihi za wajumbe ambayo zote zinakuwa zimeghushiwa.
“Halafu mwakani mnataka viongozi wa namna hiyo turudishe majina yao, hatuwezi kuwarudisha kamwe watu waliosababisha migogoro hiyo,”alisema.
Mwenyekiti alisema CCM haiwezi kukubali kuona migogoro ya ardhi inaendelea kushika kasi katika maeneo mbalimbali mkoani hapa na akasisitiza ni vizuri Viongozi wakafuata taratibu.
“Mwekezaji anapotaka ardhi anawasilisha ombi Serikali ya kijiji kisha wanakaa wanajadili wanapeleka kwenye mkutano mkuu ambao ndiyo unaoamua kutoa ardhi hiyo…Tena kwa mamlaka mliyokuwa nayo hazizidi ekari 50,” alisema Mwenyekiti huyo na kuongeza kwamba viongozi wengi hawafuati taratibu hizo.
Alisema CCM Mkoani Tanga itahakikisha haitarudisha majina ya Wenyeviti ambao wamesababisha migogoro hiyo ambayo imsababisha malalamiko kutoka kwa wananchi.
Kufuatia hatua hiyo, Mwenyekiti huyo amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Abel Busalama kufutilia watu wote waliochukua ardhi bila kufuata utaratibu na kuirejesha Serikalini.
“Mkuu wa wilaya na kamati yako ya Ulinzi na Usalama wafuatilieni wale wote waliopata Ardhi kinyume cha utaratibu na ardhi hiyo irudishwe Serikali,” alisema.