Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya jumanne iliwasilisha malalamishi mengine rasmi, kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), kuitaka kuhakikisha kwamba inaangazia kile inachokiita uporaji wa kimfumo, wa maliasili zake, mashariki mwa nchi hiyo.
DRC inasema uhalifu huo unafanywa na wanajeshi wa Ulinzi wa Rwanda (RDF) na waasi wa kikundi cha waasi cha M23.
ICC tayari ina uchunguzi unaoendelea mashariki mwa Kongo tangu 2004 na haijabainika kama mashtaka hayo mapya yatabadilisha mwelekeo wa mahakama hiyo.
Wizara ya Sheria ya Kongo ilisema katika taarifa yake kwamba. “Serikali ya DRC inasalia na wasiwasi mkubwa kuhusu mateso ya wakazi katika sehemu ya eneo lake iliyoathiriwa na vitendo vilivyorejelewa katika kesi hii,”
Taarifa hiyo imeongeza pia kwamba, Lengo la mashtaka hayo itakuwa kuchunguza na kumfungulia mashtaka mtu yeyote aliyehusika katika ukiukaji wa haki za binadamu kati ya 2022 na 2023.
Kundi la waasi la M23 linaloongozwa na watu kutoka kabila la Watutsi lilianzisha mashambulio mapya mashariki mwa Kongo mwezi Machi mwaka jana, na kuteka miji na vijiji katika eneo linalopakana na Uganda. Mapigano hayo yalilazimisha zaidi ya watu milioni 1 kukimbia makazi yao.
Kongo imeishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuunga mkono kundi la M23. Serikali ya Rwanda imekanusha shutuma hizo.