Wananchi wa kijiji cha Msamvu kilichopo kata ya Tunguli wilayani Kilindi mkoani Tanga, wameiomba serikali iharakishe kumaliza kituo cha afya ili kuokoa maisha ya wakazi zaidi ya 7,000 wanaohitaji huduma za afya.
Wakitoa malalamiko yao kwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajab Abdulhaman Abdallah aliyeanza ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya chama, walisema kukosekana kwa kituo cha afya licha ya kutokea vifo lakini pia wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 90 kufuata huduma hiyo katika hospital ya Berega iliyopo Gairo mkoani Morogoro.
“Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM tunaomba chama na serikali itusaidie, kituo cheti cha afya kikamilike maana kuna vifo vinatokea lakini pia tunatembea umbali mrefu hadi hospital ya Berega iliyopo mkoa mwingine, wajawazito na watoto kama huna shilingi laki moja kwenda hospital ya Berega wanakufa,” alisema Halima Omari.
Ofisa mtendaji wa kata ya Tunguli, Omari Mtoi alisema awali mwaka 2021 serikali ilileta fedha kiasi cha shilingi milioni 400 lakini hazikutumika hadi zikarudishwa hazina na kisha fedha hizo zikarudishwa tena mwaka wa fedha uliofuata.
Alisema jengo hilo bado halijakamilika kutokana na changamoto mbalimba ingawa fedha za kumalizia ujenzi bado zipo.
“Mheshimiwa Mwenyekiti ujenzi wa kumalizia mradi huu wa kituo cha afya ulikumbumbwa na changamoto ikiwemo mvua lakini pia uletaji wa vifaa, fedha zake zipo za kumalizia,” alisema mtendaji huyo.
Akizungumza na wananchi hao, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Ustadh Rajab alisema kwakuwa fedha za kukamilika kwa mradi huo zipo ametoa mwezi mmoja uwe umekamilika na kutoa huduma kwa wananchi.
Alisema mara nyingi wananchi wanailalamikia serikali pamoja na CCM lakini malalamiko hayo yanasababishwa na watendaji ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao licha ya serikali kutoa fedha nyingi.
“Dkt Samia Suluhu Hassan hawezi kukubali hilo wananchi wafuate huduma umbali mrefu lazima tutoe majawabu kwa wananchi wetu katika maeneo tunayo yasimamia kuepuka malalamiko yasiyokuwa na msingi kutoka kwa wananchi,” alisema Mwenyekiti huyo.
Wakati huo huo, Mwenyekiti huyo aliyeongoza na Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Tanga Mohamed salim ‘Ratco’ walitoa kiasi cha sh. 1,950,000 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mheza kilichopo kata ya Masagalu fedha ambayo itawezesha zahati hiyo kukamilika.
Pia Mwenyekiti huyo alitoa kiasi cha shilingi 680,000 kwa ajili ya kununua mifuko 40 ya kumalizia ujenzi wa ofisi ya CCM kata ya Kikunde.