Kila Mei 28, duniani kote wadau wa afya na jinsia huadhimisha siku ya hedhi duniani.
Shirika la WaterAid Tanzania liliungana pamoja na wanafunzi na walimu katika shule ya Misima iliyoko halmashauri ya mji wa Handeni katika hafla ya kukabidhi mradi wa ukarabati wa miundombinu ya maji na mafunzo tabia siha uliofadhiliwa na shirika la Hilton Global Foundation pamoja na WaterAid ili kupunguza makali ya ukosefu wa maji katika shule hiyo hasa kwa watoto wa kike wanapokua katika kipindi cha hedhi.
Sambamba na ukarabati wa huduma za maji na tabia siha, Mkurugenzi wa Shirika la WaterAid Tanzania Bi Anna Mzinga alimkabidhi mkuu wa shule cherehani moja kwa ajili ya wanafunzi kujishonea pedi za kitambaa, vifaa 40 vya kushonea pedi, katoni 55 za pedi (kutumika katika kipindi cha mvua pale pedi za kufua zitashindwa kukauka), vifaa vya michezo seti 3, mabango 20 kwa ajili ya kujifunza masuala ya usafi na televisheni kwa ajili ya kujifunza tabia siha na usafi kwa ujumla.
Bi. Anna Mzinga alisema….“tumefanikisha ukarabati wa miundombinu kadhaa ya mfumo wa maji, matenki la kuhifadhia maji, vyoo ikiwemo kuweka muundombinu wa choo rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na zaidi ya yote kutoa elimu kuhusu usafi kwa wasichana na wavulana katika hatua za makuzi yao binafsi hii ilijumuisha mafunzo maalumu ya namna ya kujitengezea taulo za kike za kujisitiri wakati wa hedhi ili kujilinda na adha mbalimbali wanapokua katika kipindi cha hedhi.”
Akiongea katika hafla hii iliyofanyika shule ya Misima wilayani Handeni , Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Handeni Ndg Upendo Magashi alisisitiza:
“ Miundombinu hii inahitaji kutunzwa ili iweze kutoa huduma husika kwa kipindi kirefu kwa sasa na kwa wanafunzi watakaokuja kusoma katika shule hii hivyo haina budi itunzwe”
Licha ya kwamba jitihada za dhati zimefanyika na Serikali pamoja na wadau ila bado inaripotiwa kwamba 34% ya wasichana hukosa vipindi shule kutokana na upungufu wa vyumba maalumu vya kujisitiri wakati wa hedhi huku 26% kutokana na ukosefu wa maji na vyoo safi katika shule.
Wito wa shirika la WaterAid wadau wote kupitia kauli mbiu ya kitaifa ya siku ya hedhi..“Hedhi ni tunu na Msingi wa Afya kwa wasichana na Wanawake, Tuiwezeshe” ni kuendelea kuweka mkazo katika masuala ya hedhi iliyo salama kwa wasichana na wakina mama kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.