Mbunge wa Kwimba, Shanif Mansoor alikuwa wa pili kuchangia katika #BajetiYaNishati. Katika mchango wake, Mansoor alimpongeza sana Waziri January Makamba na watendaji wa Wizara hiyo kwa kazi kubwa wanayofanya kiasi cha kuondoa kelele nyingi zilizokuwepo katika Wizara hiyo.
“Inaonekana kazi nzuri, mwaka huu Mheshimiwa Waziri umekuja hapa hakuna kelele kwenye Wizara ya Nishati, nakumbuka mwaka jana ulipofika hapa (kulikuwa na kelele)” alisema Mansoor.
Kwa upande wake Waziri January Makamba wakati akisoma hotuba yake ya bajeti, alisema anatambua kuwa Wizara anayoongoza ina maneno mengi na amewashukuru Wabunge kwa kuendelea kuwashauri. Pia alisema Wabunge wamemvumilia katika kipindi chote, na sasa mambo yameanza kukaa sawa.
‘Ninayo furaha kubwa kukuarifu Bunge lako tukufu, Wiki moja kuanzia sasa Bwawa letu la Mwalimu Nyerere litafikisha kiwango cha chini cha kuweza kuzalisha umeme‘ – Waziri wa Nishati, January Makamba
‘Kwa mara ya kwanza tutaingiza umeme wa jua wa Megawati 50 kwenye gridi ya Taifa, Juzi tumesaini mkataba kwa ajili hiyo. Mradi huu uko Kishapu Mkoani Shinyanga’ – Waziri wa Nishati, January Makamba
‘Serikali itachukua hatua za dharura za kuimalisha upatikanaji wa umeme mkoa wa Mtwara, tumekaa na Wabunge wa Mtwara na tumekubaliana hatua za kuchukua’ – Waziri wa Nishati, January Makamba
‘Nawashukuru sana Wabunge, Wizara yetu (ya nishati) ina maneno mengi, mmetushauri vizuri na mmekuwa na subira na sisi mpaka mambo yameenda vizuri’ – Waziri wa Nishati, January Makamba