Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaomba Watanzania kuiombea Timu ya Yanga ili iweze kushinda katika mchezo wake wa pili wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria ili warudi na kombe.
Waziri Mkuu ameyasema hayo asubuhi Bungeni Jijini Dodoma leo wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kwa kuitakia kila la heri Yanga SC ambayo inaondoka asubuhi hii kuelekea Algeria kwa ajili ya mchezo huo.
Aidha Waziri Mkuu Majaliwa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ndege aina ya Dreamliner kwa ajili ya kuwapeleka Wachezaji, Viongozi, Mashabiki na Viongozi wa Serikali ambao wataisindikiza Yanga kwenye mashindano ya Fainali hiyo
Kikosi cha Young Africans kimeondoka hii leo kuelekea nchini Algeria huku uongozi wa Young Africans ukitamba kuwa unakwenda kuishangaza Afrika kwa kutwaa ubingwa wa michauno hiyo dhidi ya USM Alger, katika mchezo huo utakaopigwa Jumamosi (Juni 03), kikiwa na deni la kupoteza mchezo wa Mkondo wa Kwanza kwa kufungwa 2-1, hivyo kitalazimika kusaka ushindi wa 2-0 ama zaidi ili kujihakikishia ubingwa wa Afrika msimu huu
Afisa Mtendaji Mkuu wa Young Africans, Andre Mtine amesema: “Bila kujali matokeo ya mchezo wetu wa kwanza tunajivunia hatua kubwa kama timu ambayo tumefanikiwa kufika kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.