Ni June 1, 2023 ambapo Waziri wa Nishati, January Makamba amehitimisha Mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Nishati.
“Rais wa awamu ya sita alivyoingia madarakani akatupa hii kazi, umeme ukawa unakatika katika tukaanza kunyooshewa vidole “Ni yule bwana KIPARA pale ndio anakata umeme, na ni Bwana Maharage (Chande) ndio anakata umeme”. Sisi tulichofanya tukajifungia na wataalam wale mnaowaona. Tukawaambia hebu tuambieni ukweli. Maana kulikuwa na dhana kwamba ni hujuma, mimi siamini kabisa kwamba mtu ameajiriwa TANESCO ahujumu umeme kwa kukata umeme kwa sababu ndio maisha yake”- Waziri wa Nishati, January Makamba.
Amesema wataalam walifanya uchambuzi na kuja na mradi wa GRIDI IMARA ambao anaamini utamaliza changamoto ya kukatika kwa umeme katika miaka ijayo.
“Mradi wa megawati 80 hapo Mtera, umejengwa kwa miaka 6. Mradi wa Julius Nyerere (Megawati 2115) tulipanga kujenga kwa miaka 3. Sasa CAG alitusema kwamba hakukuwa na ukadiriaji sahihi wa muda wa ujenzi wa mradi na alikuwa sahihi. Hakuna mahala popote unaweza kujenga megawati 2115 kwa miaka 3. Huo ndio ukweli. Mchungu lakini ukweli” Waziri wa Nishati, January Makamba.