Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu leo tarehe 02 Juni 2023 akiwa Bukoba Mkoani Kagera ametangaza kuwa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg umekwisha rasmi Tanzania.
“Kwa mujibu wa miongozo ya Shirika la Afya la Duniani (WHO), tangu tulipomruhusu mgonjwa wa mwisho, tulipaswa kuendelea kuchukua hatua za udhibiti ikiwemo ufuatiliaji wa tetesi katika jamii na kuchunguza Wahisiwa wote kwa siku 42 tangu mgonjwa wa mwisho alipopona Virusi vya Marburg, kwa hesabu hizo, ilipofika juzi tarehe 31 Mei 2023, tulifikisha siku 42 tangu mgonjwa wa mwisho kupona Virusi vya Marburg, na hivyo kukidhi vigezo vya WHO vya kutangaza mwisho wa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg”
“Nawakumbusha Wananchi wote kuwa, kumalizika kwa mlipuko huu isiwe mwisho wa kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza kama inavyoelekezwa na Wataalamu wa Afya na kwa Wataalamu wa Afya tuendelee kuchukua tahadhari wakati wote
Shirika la Afya duniani kupitia kwa mwakilishi wake nchini Tanzania Dr. Zabron Yoti wametoa pongezi kwa Tanzania kwa namna serikali ilivyochukua hatua za haraka na kufanikiwa kuzuia maambukizi kutosambaa nchini Tanzania na duniani kwa ujumla.
Pamoja na hayo Umoja wa Afrika na chake cha udhibiti wa magonjwa Africa CDC kupitia kwa kaimu mkurugenzi wake nchini Tanzania Dr. Ahmed Ogwell Ouma pamoja na kupongeza kwa namna nchi za Afrika zinavyoshirikiana, amehimiza nchi za Afrika Mashariki kuwa na mpango wa pamoja wa kushughulikia magonjwa ya milipuko.
Ugonjwa wa Marburg umewahi kuikumba nchi ya Uganda kwa mara saba katika nyakati tofauti na kufanikiwa kuudhibiti hali inayoziamsha taasisi za utafiti kufuatilia kwa kina kuhusu chanzo cha ugonjwa huo.