Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekubaliana kuondoa gharama ya viza kwa Watu wanaotaka kusafiri kutoka Nchi moja kwenda nyingine kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za kibiashara, ili kukuza mahusiano miongoni mwa wakazi wa Jumuiya hiyo pamoja na kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi wa Nchi husika.
Kuondolewa kwa gharama ya viza ni sehemu ya vikwazo kumi vya kibiashara visivyo vya kiforodha (NTBs) vilivyoondolewa na Jumuiya hiyo, huku vikwazo nane vikiendelea kushughulikiwa, na vikwazo vingine vipya vinne vimewasilishwa ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara baina ya Nchi hizo.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika Mkutano wa 42 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Jumuiya ya Afrika Mashariki (SCTIFI) uliofanyika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, Jijini Arusha ambapo vimeainishwa vikwazo vichache vilivyoondolewa huku vingine vikiendelea kufanyiwa marekebisho.
Mkutano huo unaojumuisha Nchi wanachama wa EAC ambao ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudani Kusini na DR – Congo, hufanyika kwa mujibu wa Kalenda ya Mikutano ya EAC ambapo kwa awamu hii Mkutano huo, uliongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Waziri wa Biashara, Uchukuzi, Viwanda na Utalii wa Burundi,Marie Chantal Nijimbere.