Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Senegal linasema karibu watu 360 walijeruhiwa katika ghasia zilizozuka siku ya Alhamisi baada ya kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.
Takribani watu 16 wanajulikana kufariki katika makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama katika mji mkuu, Dakar, na mji alikozaliwa Bw Sonko wa Zinguinchor.
Wafuasi wa Bw. Sonko wanasema kuhukumiwa kwake kwa madai ya “kifisadi” kumechochewa kisiasa.
Kwa upande mwingine serikali ya Senegal imepunguza ufikiaji wa huduma za intaneti na simu za mkononi katika baadhi ya maeneo kwa sababu ya ghasia mbaya ambapo jumbe za “chuki na uasi” zimetumwa mtandaoni.
Nchi hiyo ya Afrika Magharibi imekumbwa na maandamano na ghasia kwa muda wa siku tatu ambapo ambapo watu 16 wameuawa. Ghasia hizo ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo.
Wiki iliyopita, serikali ilizuia upatikanaji wa baadhi majukwaa ya mitandao, lakini watu wengi waliweza kujipenyeza katika mitandao iliyofungwa kwa kutumia mfumo wa VPN ambao huficha eneo la mtumiaji.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Senegal, Antoine Félix Diome amesema serikali imebana mitandao ya kijamii, ili kuzuia usambazaji wa jumbe za chuki na za kichochezi wakati huu wa fujo.
Ghasia zilizuka kwa mara ya kwanza Alhamisi, baada Ousmane Sonko kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa kupatikana na hatia ya “kuwafisidi vijana.”
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema limesaidia waandamanaji 357 waliojeruhiwa, akiwemo mwanamke mjamzito, pamoja na wanachama 36 wa vikosi vya ulinzi na usalama ambao walijeruhiwa tangu machafuko hayo kuzuka.
Kwa jumla, watu 78 waliojeruhiwa vibaya walipelekwa katika vituo vya afya, iliongeza.
Wafuasi wa Sonko na Rais Macky Sall wamebadilisha lawama kwa ghasia na vifo.