Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki amekazia hukumu ya jela inayomngoja mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie.
Kindiki alisema uhalifu wa Mackenzie ni sawa na kifungo cha maisha jela.
Akizungumza Jumapili wakati wa Ibada ya Kanisa, Waziri huyo alisema Mackenzie hatatoka gerezani kamwe,Kindiki alitangaza kwamba kufikia sasa, wamefukua miili 242 kutoka kwa ardhi kubwa ya mhubiri huyo iliyoko katika msitu wa Shakahola na kutambua makaburi mapya 22 ya halaiki.
Mackenzie aliyezuiliwa anachunguzwa kwa kushawishi waumini wake wa Kanisa la Good News International kufa njaa kwa ahadi ya uongo ya kukutana na Yesu.
“Mackenzie hatatoka jela, atazeeka humo ndani. Tunaomba Mungu ampe miaka mingi zaidi ili kuona usalama wa Kenya unaimarika. Hatatoka jela… Mackenzie atakutana na ghadhabu ya Mungu baada ya jela,” alisema.
Kindiki alisema hata mahakama ikimuachia huru Mackenzie bado atarudishwa gerezani.
Alilaumu Mahakama kwa kuwaachilia wahalifu kwa jina la kuheshimu Katiba.