Ikiwa leo ni siku ya mazingira duniani Umoja wa Mataifa imetoa wito kwa kila mtu kusaidia vita ya kutokomeza plastiki kwa faida ya mustakbali wa mazingira ya dunia na viumbe vyake.
Jamii imeombwa kutunza mazingira pamoja na kupiga vita uchafuzi wa mazingira katika fukwe za bahari ambapo kitakwimu inaelezwa kuwa dunia inazalisha tani milioni 300 za plastic kila mwaka na tani 8 mpaka tani milioni 14 huelekezwa baharini hali ambayo inapelekea kuhatarisha uhai wa viumbe ambavyo viko baharini.
Maudhui ya siku ya mazingira mwaka huu ni “tokomeza taka za plastiki”
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Antonio Guterres akiunga mkono wito huo amesema, “Kila mwaka, zaidi ya tani milioni 400 za plastiki huzalishwa duniani kote – theluthi moja ambayo hutumiwa mara moja tu. Kila siku, zaidi ya lori 2000 za takataka zilizojaa plastiki hutupwa katika bahari, mito na maziwa yetu. Matokeo yake ni janga. Chembechembe za plastiki huishia kwenye chakula tunachokula, maji tunayokunywa, na hewa tunayopumua.”
Ameongeza kuwa plastiki imetengenezwa kutokana na nishati ya kisukuku na kadiri tunavyozalisha plastiki zaidi, ndivyo mafuta ya kisukuku tunavyoyachoma, na ndivyo tunavyofanya mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi kuwa mbaya zaidi.
Hata hivyo amesema kuna suluhu “Mwaka jana, jumuiya ya kimataifa ilianza kujadili makubaliano ya kisheria ya kukomesha uchafuzi wa taka za plastiki. Hii ni hatua ya kwanza ya matumainii, lakini tunahitaji kila hatua kutekelezwa.”
Ameongeza kuwa ripoti mpya ya UNEP inaonyesha, “tunaweza kupunguza uchafuzi wa taka za plastiki kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2040 ikiwa tutachukua hatua sasa kurejeleza, kuchakata tena, kuelekeza upya, na kutenganisha plastiki.”