Leo Juni 06, 2023, Waziri wa sanaa, Utamaduni na michezo, Pindi Chana anawasilisha Bungeni Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 ya Wizara hiyo.
‘Kiswahili imekuwa Lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na ni Lugha rasmi na ya Kazi ya Umoja wa Afrika (AU). Kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya lugha hii, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limepitisha tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, ambayo kwa mara ya kwanza ilisherehekewa tarehe 7 Julai, 2022’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘BAKITA limeendesha darasa la kwanza la Kiswahili kwa walimu 49 nchini Malawi mwezi Novemba, 2022 na walimu 38 nchini Burundi mwezi Desemba, 2022. Mafunzo haya yamejenga hamasa kubwa na kusababisha walimu wa Kiswahili katika nchi hizo kuhitaji mwendelezo wa mafunzo hayo. Kutokana na vuguvugu hilo, walimu wa Burundi wameanza harakati za kuundwa kwa baraza litakalosimamia maendeleo ya Kiswahili nchini humo kutokana na hamasa waliyoipata. Aidha, BAKITA lilishirikiana na ubalozi wa Nigeria kufanikisha darasa la Kiswahili la Waandishi wa Habari 27 wa Voice of Nigeria (VON) mwishomi mwa mwezi Mei, 2023.’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
Katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Mei, 2023, BAKITA liliandaa na kurusha hewani jumla ya vipindi 891 kupitia redio na televisheni za Redio One, TBC-Taifa, TBC1, Clouds Fm, Kiss FM, U-FM, WAPO Redio, MVIWATA FM na Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya Umoja wa Mataifa. Vipindi hivi vililenga kuelimisha jamii kuzingatia matumizi fasaha na sanifu ya Kiswahili. Aidha, BAKITA liliandaa makala 49 zilizochapishwa katika gazeti la HabariLeo toleo la kila siku ya Ijumaa. Vilevile, BAKITA lilitoa jarida la mtandaoni mara 7. Jarida hili linajulikana kama Lugha ya Taifa na linatoka mara moja kwa mwezi’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘BAKITA lilitoa mafunzo kwa diaspora 42 katika nchi za Falme za Kiarabu za Abu Dhabi na Dubai, diaspora 14 katika nchi ya Italia, diaspora 28 katika nchi ya Uholanzi, diaspora 23 katika nchi ya Zimbabwe na diaspora kumi (10) nchini Nigeria. Mafunzo haya pia yanaendelea nchini Rwanda kuanzia tarehe 5 ñ 9 mwezi Juni, 2023 kwa wanafunzi 324 na mpango wa BAKITA ni kufikia balozi zote’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘BAKITA lilitoa mafunzo ndani ya nchi kwa walimu 288 sawa na ongezeko la asilimia 476 ya lengo la kufundisha walimu 50 wa kufundisha wageni. Ongezeko hilo limetokana na mbinu iliyobuniwa na BAKITA ya kutoa mafunzo hayo kwa wanafunzi wanaohitimu vyuo vikuu na lilianza kwa kuendesha kozi hiyo kwa wanafunzi 200 wa Chuo Kikuu cha Dodoma na waliobaki 88 ni wale waliofundishwa kupitia kituo cha Makao Makuu cha Ofisi za BAKITA’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘BAKITA katika kuimarisha Kiswahili kimataifa limeendelea na mradi wake wa kuunda kongoo ya Kiswahili ambapo kwa sasa kongoo hiyo ina jumla ya maneno 29,000,000 kati ya maneno 50,000,000 yanayotarajiwa, sawa na asilimia 58 ya malengo yake. Kongoo hili likikamilika litakuwa na manufaa makubwa katika uendelezaji wa lugha kiteknolojia na kuimarisha data ya uhifadhi wa lugha. Aidha, wataalamu na watu mbalimbali watakuwa na uwezo wa kulitumia kongoo hili kwa shughuli za uandishi wa kamusi, ujifunzaji wa Kiswahili na uandishi wa vitabu’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘BAKITA lilitafsiri jumla ya kazi kubwa na ndogo 954. Pia, BAKITA lilithibitisha tafsiri 2,452 zilizofanywa na Mawakala wake. BAKITA lilitoa huduma ya tafsiri na ukalimani katika mikutano miwili ya Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu huko Banjul, Gambia. Aidha, BAKITA liliratibu huduma ya ukalimani katika mikutano mbalimbali ikiwemo; Mkutano wa Tatu wa Dharura wa Baraza la Mawaziri la Afican Diamond Producers Association (ADPA), ulioandaliwa na Chama cha Wazalishaji Almasi Afrika uliofanyika Arusha, Tanzania mwezi Oktoba, 2022; Mkutano wa Baraza la Utendaji na Uratibu wa nne (4) wa nusu mwaka wa Umoja wa Afrika (AU) na Regional Economic Communities (RECs) uliofanyika Lusaka, Zambia mwezi Julai, 2022’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
“BAKITA limeandaa na kusambaza vitabu vya ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili katika nchi mbalimbali duniani. Pia, BAKITA liligawa vitabu kwa balozi 50 za Tanzania nje ya nchi ambapo kila ubalozi ulipewa vitabu 32 na vitabu vyote kwa ujumla wake viligharimu shilingi milioni 30”- Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘BAKITA lilitambua Vituo vitatu (3) vya kufundisha Kiswahili kwa wageni vikiwemo Kituo cha KKKT Shule ya Lugha Morogoro; Kijiwe cha Kiswahili cha nchini Ujerumani; Kituo cha Kiswahili na Utamaduni kilichopo Bulawayo nchini Zimbabwe na hivyo kuwa na jumla ya vituo 31 ambapo kati ya vituo, vituo 10 vilianzishwa kupitia balozi za Korea Kusini, Nigeria, Ufaransa, Italia, Sudani, Mauritius, Uholanzi, Havana, Abu Dhabi na Zimbabwe; na vituo 21 ni vituo vilivyo nje ya balozi ambavyo kati yake vituo 16 viko nchini na vitano (5) viko katika nchi za Afrika Kusini, Ethiopia, Italia, Zimbabwe na Ujerumani, (Kiambatisho Na.1). Fauka ya hayo, BAKITA limefanya utafiti na kubaini jumla ya vituo na vyuo 150 vinavyofundisha Kiswahili nje ya nchi na Watanzania zaidi ya 95 wanafanya kazi kupitia Kiswahili na taaluma zake husianifu huko ughaibuni’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘BAKITA liliendesha mafunzo kwa Wakalimani wa lugha za Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza. Aidha, kwa sasa kanzidata ya wakalimani ina wataalamu 118 wa fani hiyo ambapo 25 ni wakongwe katika tasnia na 93 ni wapya ambao walipatiwa mafunzo baada ya Serikali kununua vifaa vya kisasa vya ukalimani. Vilevile, BAKITA lilihariri na kutoa ithibati kwa vitabu 94 na Moduli saba (7) za ujifunzaji na ufundishaji kwa madarasa ya awali’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘Kituo cha Urithi wa Ukombozi kimeanzisha utalii wa maeneo ya kiukombozi yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika ambapo kwa mwaka 2022/23 zaidi ya watalii 60,152 walitembelea maeneo hayo. Kati ya watalii hao, watalii zaidi ya 152 walitoka nje ya nchi na zaidi ya watalii 60,000 walitoka ndani ya nchi na maeneo waliyotembelea ni pamoja na Mazimbu na Dakawa – Morogoro; Kongwa -Dodoma; Masonya – Ruvuma; Farm 17 na Lindi; na Kituo cha Ukombozi ñ Dar es salaam’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘Mfuko wa Utamaduni na Sanaa umefanikisha ununuzi wa vitendea kazi kwa vyuo vitano (5) vinavyozalisha wadau wapya wa Utamaduni na Sanaa katika nyanja mbalimbali hususan U-DJ, mapambo, uibuaji wa vipaji vya uimbaji, urembo, mitindo, mapambo, upishi wa vyakula vya asili n.k. Vyuo vilivyowezeshwa ni Simba Scratch Academy, Koshuma Training Institute and Co., Mwanamboka Ujuzi-HUB, Dage School of Dressing, na AM Fashion. Vyuo hivi vinazalisha wadau wapya 332 kwa mwezi mmoja wanaojishughulisha na kazi za Utamaduni na Sanaa. Aidha, Mfuko umewezesha uandishi wa miswada 12 ya filamu na tamthilia, uzalishaji wa filamu mbalimbali kama vile JERAHA, LOLITA, REHANI, KICHUGUU, ANU, ASILI YETU n.k. zinazorushwa na zinazotegemewa kurushwa katika vituo mbalimbali vya redio na luninga nchini’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani