Raia kumi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamefariki dunia katika mashambulizi ya jeshi la Sudan katika chuo kikuu cha Khartoum, serikali ya Kongo ilisema Jumatatu.
Sudan imekumbwa na mzozo wa kisiasa na kibinadamu tangu katikati ya Aprili baada ya mapigano kuzuka kati ya jeshi la kawaida na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Mji mkuu wa Khartoum umekuwa kitovu cha mapigano hayo, huku raia wamenaswa katika mapigano hayo, wakiwemo raia wa kigeni ambao bado hawajahamishwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Christophe Lutundula amesema raia wa nchi hiyo wapatao 10 wamekufa kufuatia mashambulizi ya Siku ya Jumapili, yaliyoendeshwa na Jeshi la Sudan katika kampasi ya chuo kikuu cha Kimataifa cha Afrika mjini Khartoum.
Lutundula amesema alifanya mazungumzo hapo jana na maafisa wa ubalozi wa Sudan mjini Kinshasa na kuwasilisha “ujumbe wa kero na huzuni” na kusisitiza kuwa Kongo imeomba maelezo zaidi juu ya tukio hilo pamoja na hatua kutoka kwa serikali ya Sudan ili kuruhusu kusafirishwa kwa miili hiyo.
Tangu kuanza kwa mzozo wa Sudan Aprili15, mji mkuu wa Khartoum umekuwa kitovu cha uhasama. Raia wa Sudan na wale wa kigeni wamekuwa wakinaswa katika mapigano hayo. Mzozo huo kati ya majenerali wawili hasimu tayari umesababisha vifo vya watu 1,800.