Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dkt. Pindi Chana leo amewasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa Mwaka 2023/24 Bungeni Dodoma ambapo moja ya mambo aliyoyasema kwenye hotuba yake ni kwamba hadi kufikia Aprili, 2023 Serikali imetoa mikopo yenye thamani ya Tsh. Bil 1.077 kwa Wasanii na Wadau wengine kutoka Sekta ya Utamaduni na Sanaa.
“Katika kipindi cha July, 2022 hadi Aprili, 2023, Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ulipokea maombi ya mikopo yenye thamani ya Shilingi 9,262,096,578 kutoka kwa Waombaji 219, hadi kufikia Aprili, 2023 Mfuko umefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi 1,077,000,000 kwa miradi 45 kutoka katika maeneo mbalimbali ya Sekta ya Utamaduni na Sanaa”
“Katika miradi 45 iliyowezeshwa, maeneo ya Sekta yaliyowezeshwa na idadi yake katika mabano pamoja na thamani ya fedha iliyotolewa ni Filamu (miradi 17) iliyowezeshwa Shilingi Milioni 475 Muziki (miradi 14) iliyowezeshwa Shilingi Milioni 287 Sanaa za Ufundi (miradi 5) iliyowezeshwa Shilingi Milioni 105 Sanaa za Maonesho (miradi 3) iliyowezeshwa shilingi Milioni 30 na Sanaa ya Uandishi (mradi 1) uliowezeshwa Shilingi Milioni 10, miradi hii imetoka katika mikoa saba (7) ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Mara, Iringa, Mwanza, Mtwara na Mbeya”
“Kwa umuhimu wa mikopo hii na ili kupata njia iliyo rahisi ya kuwafikia Wajasiriamali wengi wa Sekta za Wizara hii, Wizara kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ipo katika hatua za mwisho za kuingia mkataba wa utoaji wa mikopo kupitia benki ya NBC”
‘Mafanikio hayo yamechochewa na maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alichangia kwa kuziongezea morali timu zetu kwa kununua magoli ya ushindi, ambapo alianza na Sh. 5,000,000 katika hatua ya makundi na robo fainali; Sh. 10,000,000 katika hatua ya nusu fainali; na Sh. 20,000,000 na kutoa usafiri wa ndege katika hatua ya fainali. Kutokana na hamasa hiyo ya Mheshimiwa Rais, Timu ya Simba imeweza kupata jumla ya magoli 11 katika hatua ya makundi na robo fainali na kujikusanyia jumla ya Sh. 55,000,000 wakati Timu ya Yanga imeweza kupata magoli 16 katika hatua ya makundi, robo, nusu fainali na fainali na kujikusanyia jumla ya Sh. 115,000,000. Mafanikio hayo ni makubwa na ya kihistoria kwa nchi yetu kwa kuwa inaimarisha ubora wa ligi yetu na kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yetu’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘Hivi karibuni tumepokea maombi kutoka Chama cha Kriketi Tanzania (TCA) la kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kriketi ya kufuzu Kombe la Dunia kwa timu za vijana waliochini ya umri wa miaka 19 kwa nchi za Afrika. Mashindano hayo yatafanyika tarehe 21 – 30 Julai, 2023 jijini Dar es Salaam. Tunavikaribisha vyama vingine vya michezo kutoka duniani kote kuja Tanzania kufanya michezo yao, kwani ni sehemu sahihi wala hawatajutia maamuzi watakayokuwa wameyafanya ya kuichagua Tanzania’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘kwa kipindi cha Julai, 2022 hadi Mei, 2023 Serikali kupitia BMT imefanikiwa kusajili Vyama 5, Vilabu 109, Akademi 8, Vituo 10, Mawakala 4 na Wakuzaji 17. Aidha, mapitio ya Katiba ya Shirikisho ya Karate Tanzania (Tanzania Sports Karate ñ Do Federation), Chama cha Mchezo wa Gofu (Tanzania Golf Union) na Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake Tanzania yamefanyika. Pia, marekebisho ya Katiba ya Chama cha Morogoro Region Basketball Association na Katiba za Vilabu vinne (4) ambavyo ni Tanganyika Kigoma Football Club, Copco Football Club, Ceassia Queens Football Club, na Rock Solution Football Club yamefanyika’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘BMT limefanikiwa kujenga Mfumo wa Usajili wa kidigitali (Online Registration) wenye lengo la kurahisisha utaratibu wa usajili kwa watendaji na wadau wa michezo. Mfumo huu utasaidia shughuli za usajili kufanyika kidigitali. Mfumo huu utawarahisishia wadau wa michezo kufanya usajili mahali popote walipo na kuwezesha kufanya malipo kwa kupata namba ya kumbukumbu ya malipo (control number). Kadhalika, mfumo huu utasaidia kuongezeka kwa ukusanyaji wa maduhuli. Kwa sasa mfumo upo kwenye hatua ya majaribio’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘Katika kuendeleza dhana ya utawala bora kwa vyama, BMT limeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuandaa Katiba za mfano kwa vyama, vituo, wakuzaji, mawakala wa michezo, kufanya chaguzi za vyama mbalimbali vya michezo. Vyama vilivyofanya chaguzi ni pamoja na Tanzania Baseball & Soft Ball Association (TaBSA); Tanzania Rugby Union (TRU); Tanzania Table Tennis Association (TTTA); Tanzania Hockey Association (THA); Tanzania Golf Union (TGU), Tanzania Ladies Golf Union (TLGU), Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA)na Athletics Tanzania (AT)’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Serikali wamejiunga na programu maalumu ya Mpira wa Miguu kwa Shule ìFootball for Schools(F4S)î inayodhaminiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Dunia (FIFA) ambapo Tanzania itapokea mipira takriban elfu sitini na nne (64,000) kwa ajili ya programu hiyo. Mipira hiyo itapelekwa katika shule za Msingi zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar ambapo kila Mkoa utapokea mipira takriban elfu mbili (2,000)’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani