Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ngara iliyopo Mkoani Kagera imetia saini mkataba wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii wenye thamani ya shilingi 257,693,700 kati yao na kampuni ya Tembo Nickel ambayo inatarajia kuanza zoezi la kuchimba madini katika mgodi wa madini ya Nickel uliopo Kabanga Wilayani humo,na fedha hizo ni kwa ajili ya miradi ya Elimu na Afya.
Akiongea kwa niaba ya Tembo Nickel,Afisa Mtendaji Mkuu Manny Ramos amesema kuwa mkataba huo umesainiwa ikiwa ni mwezi mmoja umepita tangu walipokabidhi kwa mafanikio makubwa miradi ya mwaka 2022 ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii wilayani Ngara ambayo ilikuwa na thamani ya shilingi 208,111,092 katika sekita mbili.
Aidha amesema kuwa kwa sasa bado hawajaanza uzalishaji wala kupata faida lakini nia yao ni kuendelea kuchangia kadri ya uwezo wao kwenye maeneo muhimu kwa jamii na wadau wao kwa ujumla.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ngara Vedasto Tibaijuka ambaye ameshuhudia zoezo hilo ameipongeza kampuni ya Tembo Nickel kwa kujitoa kusaidia Jamii ya Wilaya ya Ngara huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa yale waliyokubaliana na kuhakikisha wanakamilisha miradi hiyo kwa muda uliopangwa ili ianze kufanya kazi.