Taarifa iliyotolewa jana na Shirika la Afya Duniani (WHO) imeeleza kuwa, hakuna kesi mpya zilizoripotiwa katika siku 42 zilizopita nchini humo baada ya mgonjwa wa mwisho kuruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kupatiwa matibabu.
Dr Matshidiso Moeti Mkurugenzi wa Kikanda wa WHO barani Afrika ameeleza kuwa kazi kubwa iliyofanywa na wafanyakazi wa sekta ya afya wa Guinea ya Ikweta na msaada wa taasisi washirika vimekuwa muhimu sana katika kusaidia kutokomeza mlipuko wa homa ya Marburg nchini humo.
Kesi 17 ziliripotiwa katika mlipuko wa kwanza wa homa ya Marburg huko Equatorial Guinea ambazo zilithibitishwa kimaabara huku watu wengine 23 wakishukiwa kuambukizwa virusi vya ugonjwa huo katika taifa hilo la Afrika ya kati lenye wakaazi milioni 1.6 tangu kuanza mlipuko huo Februari 13 mwaka huu.
Taarifa ya Shirika la Afya Duniani imeongeza kuwa, kurpotiwa vifo 12 vilivyosababisha na homa ya Marburg huko Equatorial Guinea kati ya kesi zilizothibitishwa, huku watu wengine 23 ambao walishukiwa kupatwa na homa hiyo pia waliaga dunia katika wilaya tano za majimbo nane ya nchi hiyo.
Virusi vya Marburg ni pathojeni hatari ambayo husababisha homa kali mara nyingi huambatana na kutokwa na damu kunakoathiri viungo vingi na kupunguza uwezo wa mwili kufanya kazi vizuri. Ni sehemu ya familia ya filovirus, ambayo virusi vya Ebola pia vinapatikana.
Guinea ya Ikweta imetangazwa kuwa bila ya mlipuko wa virusi hatari vya Marburg, miezi minne baada ya homa yenye kuambukiza pakubwa ya virusi vya haemorrhagic kuthibitishwa kwa mara ya kwanza nchini humo.