Watu 42 wanaodaiwa kushindwa kulipa kodi ya Ardhi Mkoani Geita wamefikishwa katika Mabalaza ya Ardhi kwa ajili kulipa kodi hizo huku 15 kati yao wakidaiwa kulipa kodi hiyo ndani ya kipindi ambacho tayari walikuwa wameshafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Akizungumza na wandishi wa habari Mara baada ya kuwafikisha wadaiwa sugu hao wa Kodi ya Pango la Ardhi katika Vyombo vya Sheria , Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Geita Rugambwa Banyikila amesema ni wajibu wa kila Mwananchi kulipa kodi ya Ardhi kwani ni Jukumu la Kisheria.
“Wananchi wote kutoka Halmashauri zote sita za Mkoa huu wa Geita ambao wanamiriki viwanja na Mashamba waweze kulipa Kodi zao za Ardhi kwani kwa sasa utaratibu wa kuwafikisha wale wadaiwa sugu katika Vyombo vya kisheria kwenye Baraza yetu ya Ardhi unaendelea na Mpaka sasa tunawadaiwa takribani 42 ambao wameshafikishwa kwenye vyombo vya kisheria kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanalipa kodi ya pango la Ardhi , ” Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Geita.
Banyikila amesema kuna maeneo ambayo yamepimwa viwanja na wananchi wengi wamekuwa hawajitokezi kuja kumilikishwa maeneo huku akiwaomba wananchi wa Mkoa wa Geita kujitokeza kwa ajili ya kwenda kumilikishwa viwanja hivyo huku wakiendelea na utaratibu wa kwenda kuwafata wananchi kwa kuwaandalia hati.
Kamishina Msaidizi Banyikila amesema zoezi la utoaji hati katika kata ya Bwanga linaanza tarehe 15 ya Mwezi huu na watakuwa wakitoa hati kwa wananchi huku akiwataka wananchi wa Bwanga kuwa tayari kwa ajili ya kupokea hati hizo na kuwakumbusha yale maeneo yote ambayo wamekwisha kufanya utoaji wa Elimu kwa ajili ya Maandalizi ya hati katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Buselesele kuweka kambi huku wananchi hawakujitokeza.