Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makale Mbarawa, amewasilisha Azimio la Bunge kuhusu pendekezo la kuridhiwa mkataba baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa lengo la kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika uendelezaji wa maeneo ya Bandari Nchini.
Mhe. Mbarawa, amesema Mkataba huu umeainishwa katika awamu kuu mbili za maeneo ya ushirikiano. Awamu ya kwanza itajumuisha: kusimamia, kuendesha na kuendeleza baadhi ya Magati katika Bandari ya Dar es Salaam; kuboresha Gati la Majahazi na Gati la Abiria katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuvutia vyombo vikubwa zaidi na meli za kitalii kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam; kuwekeza katika maeneo yaliyotengwa katika Bandari Kavu; kufanya uwekezaji katika Mifumo ya Kisasa ya TEHAMA ya kuendeshea shughuli za kibandari ili kuongeza ufanisi wa Bandari kuwa shindani; na kuwajengea uwezo Watumishi wa TPA ili waweze kutekeleza shughuli za Bandari kwa ufanisi katika maeneo mengine ya Bandari Nchini. Msisitizo wa Serikali ni kuhakikisha maeneo yote ya nchi yanabaki chini ya umiliki wa Serikali.
Pia awamu ya Pili ya Miradi, majadiliano yatafanyika kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo: kuongeza thamani ya bidhaa, maeneo ya viwanda na miundombinu mingine itakayoongeza ufanisi katika usafirishaji wa bidhaa kwenda na kutoka nchi zinazotuzunguka, kuwekeza katika Bandari zingine za Bahari na Maziwa kama itavyopendekezwa na Serikali kupitia TPA kwa kuzingatia ulinzi na maslahi mapana ya Taifa na kuwekeza katika vyombo vya usafirishaji wa shehena (matishari) katika maziwa makuu, ili kuunganisha bandari za Maziwa Makuu na bandari za nchi jirani kama itakavyopendekezwa na TPA na kukubaliana na Mwekezaji.