Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makale Mbarawa, amesema iwapo Bunge la Tanzania litaridhia Azimio hilo na kuwezesha Serikali kuendelea na hatua zinazofuata za majadiliano na Serikali ya Dubai, hihi ndizo baadhi ya manufaa yatakayopatikana;
* Kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 kwa sasa mpaka masaa 24. Hii itapunguza gharama za utumiaji wa Bandari yetu. Matokeo yake itaongeza idadi ya meli zitazokuja Bandari ya Dar es Salaam kutoka meli 1,569 zilizohudumiwa mwaka 2021/22 mpaka kufikia takriban meli 2,950 ifikapo mwaka 2032/33.
* Kupunguza muda wa ushushaji wa makontena kutoka siku 4.5 mpaka siku 2.
* Kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka masaa 12 mpaka saa 1 kutokana na uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA.
* Kupunguza gharama ya usafirishaji wa mizigo kutoka nchi za nje kwenda nchi za Jirani, kwa mfano kutoka US$ 12,000 mpaka kati ya US$6,000 na US$7,000 kwa kasha linalokwenda nchi ya Malawi, Zambia au DRC. Hii italeta Watumiaji wengi kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
* Kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 18.41 za mwaka 2021/22 hadi kufikia tani milioni 47.57 mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 158.
* Kuongezeka kwa Mapato ya Serikali yatokanayo na Kodi ya Forodha inayokusanywa katika shehena inayopitishwa bandarini kutoka Shilingi Trilioni 7.76 za mwaka 2021/22 hadi Shilingi Trilioni 26.7 za mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 244.
* Kuongezeka kwa ajira zinazotokana na shughuli za bandari kutoka 28,990 mwaka 2021/22 hadi ajira 71,907 ifikapo mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 148.