Waziri wa Ujenzi Prof. Makame Mbarawa leo June 10,2023 amewasilisha Bungeni maelezo ya awali kuhusu mapendekezo ya kuridhia mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa Bandari Tanzania ambapo amesema waliamua kuchagua kufanya majadiliano na Kampuni ya DP World kwakuaa ina uzoefu wa kuendesha Bandari sita Afrika na Bandari zaidi ya 30 Duniani kote kwa ufanisi mkubwa.
“Mkataba huu hauna masharti yanayoifunga Serikali kuhusu maeneo ya ushirikiano yaliyoanishwa pasipo uwepo wa mikataba mahsusi wa utekelezaji wa miradi itayojadiliwa na kukubaliwa na pande mbili.” – Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa
“Mkataba huu inaitaka DP World kuendeleza ajira za watumishi wote waliopo, kuwaajiri Watanzania pamoja kuwaendeleza kitaaluma. Vilevile, mkataba huu umeweka bayana sharti kwa Kampuni ya DP World kutumia wakandarasi wa ndani katika manunuzi ya huduma na bidhaa pamoja na kusaidia vyuo vya mafunzo vya Tanzania katika masuala ya elimu ya usafirishaji majini.” – Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Makame Mbarawa
“Mkataba huu unatoa haki ya upekee ya kufanya majadiliano kwa awamu ya miradi iliyoanishwa kwenye mkataba huo kwa kipindi kisichozidi miezi kumi na mbili. Msingi wa kutoa haki hii ya kipekee ni kuwezesha pande mbili kufanya majadiliano na kumpa uhakika mwekezaji kujadiliana katika maeneo pasipo kuwepo kwa majadiliano na mwekezaji mwingine katika maeneo hayo hayo.
Hivyo, iwapo kipindi hicho kitakwisha bila kufikia makubaliano, TPA inaweza kuanzisha majadiliano na wawekezaji wengine katika maeneo hayo pasipo kuwepo kwa mgogoro wowote chini ya mkataba huo.” – Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Makame Mbarawa