Ofisi ya Rais wa Kenya William Ruto imetangaza kwamba Djibouti na Kenya zimekubaliana kuondoa mahitaji ya viza kwa raia wao.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, afisi hiyo ilisema mataifa hayo mawili ya Afrika mashariki yanatumai kuendeleza biashara yao ya pande mbili chini ya msukumo wa mfumo wa kutokuwepo kwa viza kwa raia wa upande mwingine.
Kwa hatua hiyo ya kufuta mahitaji ya viza kwa raia wao, nchi hizo mbili pia zinatumai kuimarisha uhusiano wa uwekezaji kati yao pamoja na kuimarisha utulivu wa kikanda.
Makubaliano hayo yalifikiwa mapema Jumapili kwenye mkutano kati ya Rais wa Kenya William Ruto na mwenzake wa Djibouti Ismail Omar Guelleh uliofanyika katika mji wa Djibouti.
Ofisi ya rais wa Kenya pia ilibainisha kuwa viongozi hao wawili walijadili kuanzishwa tena kwa usafiri wa anga kati ya Nairobi na mji wa Djibouti.
Kwa sasa Ruto yuko nchini Djibouti kuhudhuria Mkutano wa 14 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) unaofanyika mjini Djibouti kuanzia leo Jumatatu.
Ruto zaidi alisema utawala wake na serikali ya Djibouti wanakamilisha mipango ya kurejesha safari za ndege za moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili.
“Kurejeshwa kwa muunganisho wa anga bila shaka kutakuwa na athari kubwa katika kuimarisha biashara kati ya mataifa yetu mawili,” alisema.
Ruto pia alisema Kenya inafanya kazi kwa karibu na Djibouti katika sekta ya elimu, na kuahidi kuwaruhusu wanafunzi 300 wa Djibouti kujiunga na vyuo vikuu vya Kenya. Alisema wanafunzi hao wa kigeni watalipa karo sawa na Wakenya.
Sekta nyingine zitakazofaidika kutokana na ushirikiano wa nchi hizo mbili, kulingana na kiongozi huyo wa Kenya, ni nishati, sanaa, masuala ya vijana na utalii.
Alisema Djibouti imeruhusu kampuni ya nishati ya Kenya kuchimba visima viwili vya jotoardhi nchini, huku awamu ya kwanza ya mradi ikiwa tayari imekamilika.