Sijawahi kuona boti imeshika moto tena Watu wakiwa nayo baharini na wala siombei hiyo itokee kwa yeyote, nikiitazama hii picha naendelea kujiuliza hata hawa waliookolewa walitokajetokaje kwenye balaa kama hili ? vipi kama wenye Boti wangekuwa wamechukulia poa na kutembea bila vifaa vya uokoaji kama vile life jackets ? …..wakati maswali yakiwa mengi kuhusu ajali hii hizi ndio taarifa zilizopo hadi sasa.
Waokoaji Nchini Misri wanawatafuta Watalii watatu wa Uingereza ambao hawajulikani walipo baada ya moto kuzuka kwenye Boti waliyokuwa wakisafiria baharini nchini Misri jana Jumapili.
Vyombo vya habari vya Misri vimesema Boti hiyo ya Watalii ilikuwa imebeba jumla ya Watu 27 huku miongoni mwao ni Watalii 15 wa Ungereza ambapo Waingereza 12 waliokolewa na sasa kazi imebaki ni kuwatafuta watatu wasiojulikana waliko.
Tukio hilo limetokea siku chache baada ya fukwe kufungwa katika eneo la mapumziko la Bahari Nyekundu la Hurghada baada ya Mwanamume Raia wa Urusi aliyekuwa akiogelea baharini kufariki baada ya kutafunwa na papa.
Utawala wa Bahari Nyekundu nchini Misri umesema wafanyakazi 12 na watalii 12 wa Uingereza waliokolewa nje ya mji wa mapumziko wa kusini mwa Bahari Nyekundu wa Marsa Alam.