Mwanamume mmoja muingereza alijaribu kupanda jengo la tano kwa urefu duniani bila kamba siku ya Jumatatu, na kusababisha mamlaka ya Korea Kusini kumlazimisha kuacha kupanda zaidi ya nusu ya mnara wa Lotte World wa ghorofa 123 huko Seoul kwa kuwa ni hatari .
Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 24, akiwa amevalia kaptula, alipanda juu ya jengo hilo la kihistoria kwa zaidi ya saa moja huku polisi na kikosi cha zima moto wakiwa wamekusanyika chini kumtaka ashuke.
Alifika ghorofa ya 73 ambapo mamlaka ilimlazimisha kurudi na kuingia ndani ya jengo hilo, afisa wa idara ya zima moto alisema, akiongeza kuwa polisi walimkamata kwa mahojiano lakini polisi hawakupatikana mara moja kutoa maoni yao.
Gazeti la Chosun Ilbo lilimtaja mtu huyo kuwa George King-Thompson.
Vyombo vya habari vya Uingereza viliwahi kuripoti kwa mtu aliye kamatwa na kufungwa jela kwa kupanda jengo la Shard huko London mnamo 2019.
Mnamo 2018 polisi walimkamata “Spiderman wa Ufaransa” Alain Robert akiwa zaidi ya nusu ya Mnara wa Ulimwengu wa Lotte.