Miamba wa Misri, Al Ahly walipata bao la dakika za lala salama na kupata sare ya 1-1 katika mchezo wa mkondo wa pili wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumapili na kutwaa taji hilo huku wakiwaondoa mabingwa Wydad Casablanca ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-2.
Wydad Casablanca ya Morocco na Al Ahly ya Misri siku ya Jumapili waliendeleza vita vyao vya kutafuta mfalme wa klabu za soka barani Afrika, walipokutana katika mkondo wa pili wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya CAF uliopigwa kwenye Uwanja wa Stade Mohamed V mjini Casablanca.
Wenyeji Wydad walikuwa wa kwanza kucheka n nyavu kupitia goli la mapema la Yahya Attiatullah kunako dakika ya 27. Mafarao walitoka nyuma na kupata bao la kusawazisha, ambalo kimsingi lilikuwa la ushindi, katika dakika ya 78 ya mchezo kupitia kwa Muhammed Abdulmuumin.
Kwa sare hiyo Ahly wametwaa ushindi kwa jumla ya mabao 3-2.
Mechi ya kwanza katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo wikendi iliyopita ilimalizika kwa mabao 2-1 kwa upande wa Mafarao. Al Ahly, wametwaa taji la 11 la CAF Champions League lililoongeza rekodi, na la tatu katika muda wa misimu minne.