Zaidi ya watu 40 wameuawa katika shambulizi dhidi ya kambi ya wakimbizi wa ndani (IDP) kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kulingana na maafisa wa eneo hilo na wanaharakati.
Richard Dheda, afisa wa utawala wa eneo la Bahema Badjere katika eneo la Djugu katika jimbo la Ituri nchini DRC, alisema shambulio hilo kwenye kambi ya Lala mapema Jumatatu lilitekelezwa na wapiganaji wa muungano wa makundi ya wanamgambo uitwao Cooperative for the Development of the Kongo (CODECO).
CODECO inadai kulinda jamii ya Lendu kutoka kwa kabila lingine, Wahema, pamoja na jeshi la DRC.
Dheda alinukuliwa akisema na shirika la habari la AFP kwamba watu wasiopungua 41 waliuawa katika shambulio hilo kwenye kambi hiyo, iliyoko kilomita 5 kutoka Bule, eneo la kituo cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa.
Shahidi pia aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba ameona “zaidi ya miili 40” ikiwa chini.
“Walianza kufyatua risasi, watu wengi walichomwa hadi kufa katika nyumba zao, wengine waliuawa kwa mapanga,” Desire Malodra, mwakilishi wa mashirika ya kiraia, aliambia AFP.
:kwingineko
Wanachama wasiopungua 19 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameangamizwa kufuatia operesheni ya jeshi la Somalia katika eneo la kusini la Lower Shabelle.
Vyombo vya usalama vya Somalia vimethibitisha kuuawa wanachama hao wa kundi la kigaidi na kueleza kwamba, operesheni hiyo imeongozwa na Idara ya Taifa ya Intelijensia na Usalama ya Somalia (NISA).
Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, operesheni hiyo imefanyika katika kijiji cha Bula-Mohamed-Abdalla, viungani mwa mji wa Awdheegle, katika jimbo la Lower Shabelle.
Habari zaidi zinasema kuwa, magari na silaha za magaidi hao zimeharibiwa kwenye operesheni hiyo katika mji huo wa kilimo unaopatikana yapata kilomita 84 magharibi mwa Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.