Randy Cox wa Connecticut, Marekani atalipwa fidia ya dola milioni 45 (zaidi ya Tsh. Bilioni 107) baada ya kupooza mwili kulikosababishwa na kubamizwa kichwa kwenye chuma wakati akisafirishwa na gari la Polisi akiwa amefungwa pingu na bila kufungwa mkanda.
Cox aliyekamatwa June 19 2022 kwa madai ya kumtishia Mwanamke kwa bunduki, alipooza kuanzia kifuani baada ya kujigonga kichwani wakati gari hilo lilipofunga breki kali ghafla kitendo kilichomsababisha atupwe mbele na kujibamiza kwenye.
Mwanaume huyo aliwashitaki Polisi waliohusika kwenye tukio hilo pamoja na Jiji akitaka alipwe fidia ya dola milioni 100 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 237 za Tanzania lakini hadi juzi yeye na Mamlaka ya Jiji la New Haven waliafikiana alipwe hizo dola milioni 45 ambapo hata hivyo Mawakili wake wanasema ni kiwango kikubwa zaidi cha pesa kuwahi kulipwa katika kesi ya utovu wa nidhamu wa Polisi Nchini Marekani.
Mawakili wa Cox wamesema katika hizo dola milioni 45, Bima ya Jiji italipa dola milioni 30 huku Mamlaka ya Jiji hilo ikilipa kiasi kilichobaki ambapo tayari Polisi wawili waliotajwa kuhusika kwenye uzembe huo wamefukuzwa kazi na tayari wana kesi Mahakamani.