Mwanamke mwenye umri wa miaka 76 ambaye alitangazwa kufariki katika hospitali moja nchini Ecuador aliwashangaza jamaa zake kwa kugonga jeneza lake kuonesha kutaka kuamka, na kusababisha uchunguzi wa haraka katika hospitali hiyo.
“Ilitupa sisi sote hofu,” mwanawe Gilberto Barbera aliambia Associated Press, akiongeza kuwa madaktari walisema hali ya mama yake ilisalia kuwa mbaya.
Muuguzi mstaafu Bella Montoya alilazwa hospitalini siku ya Ijumaa, baada ya kupata kiharusi na mshtuko wa moyo na taarifa za kifo chake zilitangazwa na daktari wa zamu kuwa amekufa, wizara ya afya ya Ecuador ilisema.
Barbera alisema mama yake alikuwa hajitambui alipofikishwa katika chumba cha dharura na kwamba saa chache baadaye daktari alimwarifu kuwa amefariki na kumkabidhi hati za utambulisho na cheti cha kifo.
Video na picha mbalimbali zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii ilimuonyesha akiwa amelala kwenye jeneza lililo wazi na akipumua kwa nguvu huku watu kadhaa wakiwa wamemzunguka.
Wahudumu wa afya walionekana wakianza kumwangalia na kumfuatilia Bi Montoya kabla ya kumsogeza kwenye machela na kumuingiza kwenye gari la wagonjwa.
Sasa yuko katika uangalizi mahututi katika hospitali hiyo hiyo ambapo madaktari walitangaza kifo chake.
Shirika la habari la AFP lilimnukuu Bw Balberán akisema: “Kidogo kidogo ninaelewa kilichotokea sasa ninaombea tu afya ya mama yangu iendelee kuimarika ninaamtaka awe hai na awe kando yangu.”
Wizara ilisema inawachunguza madaktari ambao hawakutajwa majina waliohusika katika kesi yake, na kamati ya kiufundi imeundwa kuchunguza jinsi hospitali hiyo inavyotoa vyeti vya kifo.