Umoja wa Mataifa unasema watu zaidi ya milioni 2 nchini Sudan, wamelazimishwa kukimbia nyumba zao kutokana na vita iliyoingia mwezi wake wa pili kati ya jeshi la Serikali na wapiganaji wa RSF.
Kwa mujibu wa takwimu zisizo rasmi za mashirika ya misaada, karibu watu 959 wameuawa na wengine zaidi ya elfu 4 wamejeruhiwa mpaka kufikia Juni 12.
Shirika moja la madaktari nchini Sudan, linasema idadi hii huenda ikawa kubwa zaidi kutokana na kushindwa kupata tarifa rasmi katika maeneo kama ya el-Geneina magharibi mwa Darfur ambako mapigano yanaendelea kwa sasa.
Aidha shirika la umoja wa Mataifa linalohusika na wahamiaji, IOM linasema zaidi ya watu milioni 1 na laki 6 wamekimbia makazi yao, huku wengine zaidi ya laki 5 wakikimbilia kwenye nchi jirani za Misri, Sudan Kusini, Chad, Ethiopia, Jamuhuri ya Afrika ya Kati na Libya.
Nchi ya Sudan ilitumbukia katika machafuko April 15 mwaka huu baada ya mvutano wa kisiasa wa muda mrefu kati ya kiongozi wa kijeshi jenerali Abdel Fattha al Burhani na kamanda wa vikosi vya RSF Mohamed Hamdan Dagalo maarufu kama Hemedti.
Mapigano yameendelea tena hapo jana katika mji wa Kahrtoum na sasa kufika hata katika jimbo la Darfur, maeneo ambayo yemeshuhudia makabiliano mabaya zaidi tangu vita hiyo ianze.