Kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga anasema atawaongoza Wakenya kupinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha wa 2023 unaopendekezwa ambao anautaja kuwa wa adhabu na kurudi nyuma katika juhudi za kutokomeza umaskini nchini.
Bw. Odinga, ambaye alizuru Soko la Toi lililoko Kibra ambalo lilibomolewa Jumapili iliyopita, alikashifu masuala muhimu katika Mswada huo ikiwa ni pamoja na asilimia 16 ya ushuru wa bidhaa za petroli, ushuru wa nyumba, na fidia ya bima.
Viongozi wa Azimio waliofanya mkutano wao wa kilele Jumatano asubuhi waliwaomba Wabunge, wakiwemo wale wa Kenya Kwanza, kupiga kura dhidi ya Mswada wa Fedha na kuwaokoa wahanga hao.
“Tunajua ndani ya mioyo yenu mnajua bajeti hii ina makosa, tunawaomba muungane na wenzenu wa Azimio na kusimama na wananchi, tunawaomba akina mama mboga, wanajeneza, wana boda boda, walimu, wauguzi. madaktari, na wachuuzi miongoni mwa wengine kujiuliza, je, bajeti hii inahudumia ustawi wako?” Mwenyekiti wa azimio Wycliffe Oparanya alipendekeza.
Kiongozi huyo wa Azimio aliomba serikali ianzishe mazungumzo ya kitaifa kujadili kuhusu ushuru tata wa nyumba kwa nia ya kuwashawishi Wakenya kuunga mkono ajenda badala ya kuwashurutisha wafanyikazi na waajiri kulipa ushuru huo wa asilimia 1.5.