Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Bungeni Dodoma amewasilisha Bungeni taarifa ya Hali ya Uchumi wa Kitaifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2023/2024 ambapo moja ya mambo aliyoyasema ni kwamba Tanzania bado imeendelea kuwa Nchi ya uchumi wa kati ngazi ya chini.
“Kutokana na hatua madhubuti zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali thamani ya pato ghafi la Taifa linatarajiwa kufikia dola za Marekani bilioni 85.42 mwaka 2023/24, Mwaka 2022, pato ghafi la Taifa (kwa bei za mwaka husika) lilikuwa shilingi trilioni 170.3 (sawa na Dola za Marekeni bilioni 77.6) ikilinganishwa na shilingi trilioni 156.4 mwaka 2021 (sawa na Dola za Marekani billioni 69.94)”
“Aidha, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya Watu Tanzania Bara ilikuwa 59,851,347 ikilinganishwa na makadirio ya idadi ya Watu 57,724,380 mwaka 2021, hivyo Pato la Taifa kwa Mtu (GDP per capital) kwa mwaka 2022 lilikuwa shilingi 2,844,641 ikilinganishwa na shilingi 2,708,999 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 5.0. Kiasi hicho ni sawa na dola za Marekani 1,229.1 mwaka 2022 kwa mtu kwa mwaka ikilinganishwa na dola za Marekani 1,173.3 mwaka 2021, hali hii inaendelea kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ngazi ya chini”
‘Hadi kufikia mwezi Aprili 2023, deni la Serikali lilikuwa shilingi bilioni 79,100.19 sawa na ongezeko la 13.9% ikilinganishwa na Shilingi bilioni 69,440.01 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022.
“Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi bilioni 51,162.60 na deni la ndani ni Shilingi bilioni 27,937.59, ongezeko la deni limetokana na kupokewa kwa fedha za mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme, elimu na afya, aidha tathmini ya uhimilivu wa deni la Serikali iliyofanyika Desemba, 2022 imeonesha kuwa deni ni himilivu na viashiria vya deni viko ndani ya wigo unaokubalika kimataifa katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu” “Machi 2023, kampuni za Fitch Ratings na Moody’s Investors Service zilianza zoezi la kuifanyia Nchi tathmini ya kukopesheka katika masoko ya fedha ya kimataifa, zoezi hilo lilikamilika ambapo kampuni ya Moody’s Investors Service ilichapisha matokeo ya tathmini hiyo Mei 2023 na kampuni ya Fitch Ratings mwezi Juni 2023, kwa mujibu wa matokeo hayo, Tanzania imewekwa katika daraja la B2 POSITIVE na Kampuni ya Moody’s Investors Service na daraja la B POSITIVE na Kampuni ya Fitch Ratings ambayo yanaashiria taswira chanya kwa Nchi kimataifa”