Siku ya mtoto wa Afrika ni siku inayosherehekewa kila mwaka tarehe 16 Juni tangu mwaka 1991 ilipoteuliwa na Umoja wa Afrika katika kuenzi michango ya watoto walioshiriki katika maandamano katika mji wa Soweto, Afrika Kusini mwaka 1976 pamoja na kujengea jamii uelewa juu ya umuhimu wa elimu bora kwa watoto huku chimbuko la maadhimisho haya likiwa ni Azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990
Watoto hao walikuwa wakidai haki zao za kutobaguliwa pamoja na haki nyingine za kibinadamu ikiwemo haki ya kupata elimu bora na hivyo kupinga mifumo ya elimu ya kibaguzi hivyo ufuatia tukio hili, OAU iliazimia kuwa tarehe 16 Juni ya kila mwaka iwe Siku ya Mtoto wa Afrika.
Kupitia Maadhimisho haya, Serikali na wadau wengine tunakumbushwa kuandaa mipango thabiti ya kuwaendeleza watoto na kukuza ufahamu wa wazazi, walezi na jamii kuhusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoto wa Afrika na kuzitafutia ufumbuzi.
Aidha, maadhimisho haya ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa Sera za Taifa zinazohusu maendeleo ya watoto kwa kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na malezi bora ili kuwarithisha stadi mbalimbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na taifa kwa ujumla.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto” Kauli mbiu hii inawataka wazazi, walezi, Serikali na wadau wengine kuzingatia wajibu wetu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo ya Mtoto ili aweze kudhibiti changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.