BIlionea Elon Musk amemuajiri mtoto mwenye umri wa miaka 14 anayeaminiwa kuwa na kipaji cha kipekee na ataanza kufanya kazi kama mhandisi wa programu kwenye timu ya watengenezaji wa vyombo vya anga pamoja na satelaiti SpaceX, kampuni inayomilikiwa na Bilionea huyo. Kairan Quazi atajiunga na kampuni hiyo baada ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Santa Clara jijini California mwishoni mwa mwezi huu ambapo anatazamiwa kupokea Shahada ya Hisabati, Sayansi ya Computer na Uhandisi. (Bachelor Degree in Mathematics, Computer Science and Engineering)
Kijana huyo ameshamaliza programu ya mafunzo aliyoifanya kwenye kampuni ya teknolojia ya Intel na atafanya kazi kwenye timu ya Starlink ya SpaceX, ambayo inaunda mtandao mkubwa zaidi wa mitambo ya satelaiti.
“Starlink ni moja ya makampuni adimu ambayo hayakuchukulia umri wangu kama kizuizi na wamenichukulia kama mtu mwenye uwezo na uzoefu wa kufanya nao kazi” mtoto huyo aliandika kwenye mtandao wa LinkedIn
Wasifu alioandika kupitia mtandao wa LinkedIn tangu wakati huo umeondolewa kwani mtandao huo biashara inahitaji watumiaji kuwa na umri kuanzia miaka 16. Quazi atakuwa mhitimu mdogo zaidi katika historia ya miaka 172 ya chuo cha Santa Clara kilichopo nchini Marekani baada ya kuruka kutoka darasa la tatu hadi shule ya upili iitwayo Las Positas College alipokuwa na umri wa miaka tisa tu.
Vyombo vya habari vya nchini Marekani vimempamba mtoto huyo kwa kumuita “wonder kid” wakimaanisha ni mtoto mwenye kipaji cha ajabu kwa mafanikio yake ya kitaaluma, na vipimo vya IQ vinaonyesha kuwa yuko katika asilimia 99.9 ya idadi ya watu kwa ujumla.