Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki ameishukuru Serikali ya Ireland kwa kutoa mchango katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ya msingi.
Mhe. Kairuki ametoa pongezi hizo kwa Serikali ya Ireland kupitia kwa Balozi wake nchini Tanzania Mhe. Mary O’Neil aliyemtembelea ofisini kwake jijini Dodoma mapema leo.
Mhe. Kairuki amesema mchango wa Irelend kupitia Mfuko wa pamoja wa Sekta ya Afya (Health Basket Fund) umetoa mchango wa moja kwa moja katika uboreshaji wa huduma za afya msingi kwenye uboreshaji wa huduma, mifumo na utoaji huduma za afya kwa usawa.
Mhe. Kairuki ameainisha kuwa, mchango wa Serikali ya Ireland umeiwezesha TAMISEMI kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya afya, kuongeza rasilimaliwatu na upatikanaji wa huduma za afya katika ngazi ya msingi.
Sanjari na hilo, Mhe. Kairuki amesisitiza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendeleza ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na Ireland ili wananchi waendelee kunufaika na maboresho ya huduma za afya.