Viongozi kutoka nchi saba za Afrika walimuambia Putin kwamba, vita vinadhuru dunia nzima. Ujumbe huo ulikutana na Putin siku moja baada ya kukutana na rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky mjini Kyiv.
Putin alifungua mkutano wa Jumamosi na ujumbe wa viongozi kutoka Comoros, Jamhuri ya Congo, Afrika Kusini, Misri, Senegal, Afrika Kusini, Uganda na Zambia katika kasri moja mjini St. Petersburg, kwa kusisistiza dhamira ya Russia kufanya kazi na nchi za Afrika.
Lakini kabla ya viongozi wote kumaliza hotuba zao Putin aliingilia kati na kupinga mpango wao wa amani, unaomtaka atambuwe mipaka ya Ukraine inayotambulika kimataifa.
Alisisituza juu ya msimamo wake kwamba Ukraine na washirika wake wa Magharibi ndio walianzisha ugomvi huo muda mrefu kabla ya hata Russia kuivamia Ukraine Februari 2022.
Putin pia alisema kwamba, nchi za Magharibi ndizo za kulaumiwa kwa kuongezeka sana bei za chakula duniani tangu mapema mwaka jana, na kwamba Afrika ndio imedhurika zaidi.
Aliuambia ujumbe huo kwamba usafirishaji wa nafaka za Ukraine kutoka bahari ya Black Sea haitosaidia kamwe kupunguza matatizo ya bei za juu za chakula barani Afrika, kwa sababu sehemu kubwa ya nafaka hizo inapelekwa katika nchi tajiri.
Kiongozi wa Ukraine aliuambia ujumbe huo kwamba, kabla ya kuanza mazungumzo yeyote ya amani ni lazima Russsia iwaondoe wanajeshi wake wote kutoka ardhi ya Ukraine, jambo ambalo Moscow imesema haliweza kukubalika.