Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani vikali shambulizi la kigaidi lililoua makumi ya wanafunzi katika eneo la Mpondwe, magharibi mwa Uganda.
Farhan Haq, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema Guterres amemshtushwa na shambulizi hilo la kinyama dhidi ya shule moja katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Amesema Katibu Mkuu wa UN ameguswa na ukatili huo wa magaidi wa ADF dhidi ya wanafunzi, ambapo amezinyooshea mkono wa pole familia za wahanga wa hujuma hiyo, serikali na taifa hilo kwa ujumla kufuatia unyama huo.
Wakati huohuo, duru za habari zinaarifu kuwa, idadi ya watu waliouawa katika shambulizi hilo la usiku wa kuamkia jana Jumamosi imefika 41, aghalabu yao wakiwa ni wanafunzi.
Msemaji wa polisi ya Uganda, Fred Enanga amesema jeshi la UPDF linawafuatilia wahalifu katika Mbuga ya Taifa ya Virunga.
Wanafunzi sita waliotekwa nyara na magaidi hao
wenye makao yao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanaripotiwa kuwa katika msitu huo wa Virunga.
Wahalifu walioshambulia shule ya Sekondari ya Lubiriha Ijumaa usiku walipora na kuiba chakula na kuchoma moto mabweni ya shule hiyo iliyoko umbali wa kilomiita 2 kutoka kwenye mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.