Washiriki wapatao 500 wakiwemo wadau wakuu wa maendeleo wa Asasi za kiraia pamoja na Sekta Binafsi, wanatarajiwa kushiriki katika wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI), itakayofanyika kuanzia Oktoba 23 hadi 27, 2023 Jijini Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil Society (FCS) Francis Kiwanga ameyasema hayp alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam. Kiwanga alisema kama kauli mbiu ya wiki hiyo inavyosema, ‘ Teknolojia na Jamii’ majadiliano juu ya makutano ya teknolojia na jamii ni muhimu ili kuyalewa mabadiliko hayo Ikiwa ni pamoja na kukabiliana na changamoto zilizopo katika jamii kwa kutumia fursa zinazotolewa na teknolojia.
‘Suala kubwa tunalozungumza sisi kama wanaazaki ni kujitathmini kwa kiasi gani tumeweza kutumia teknolojia katika miradi na kazi zetu?ni maeneo gani ambayo tumejifunza au ni maeneo gani yana changamoto,?’’ alihoji.
“Tukio hili Kwa mwaka huu limejikita katika kujadili na kuweka mikakati na kuboresha utendaji wa AZAKI , kuongeza mashirikiano baina ya AZAKI na sekta binafsi na baina ya AZAKI na Serikali nchini haswa,” amesema Kiwanga.
Akifafanua zaidi, Kiwanga amesema, katika wiki hiyo kutakuwa na mada tofauti zilizojikita katika kutathimini kaulimbiu ya Teknolojia na AZAKI ambazo ni pamoja na ujumuishaji na uwekezaji wa kidigitali, matumizi ya takwimu kuleta manufaa kwa jamii, teknolojia na utetezi wa kijamii, elimu na mafunzo ya dijitali nchini Tanzania .
Aidha Kiwanga ameeleza kuwa katika wiki hiyo mijadala mbalimbali itajadiliwa, ikiwemo ya kuziwezesha na kuzipa sauti jamii za pembezoni, ujumuishwaji wa teknolojia kwenye kazi za AZAKI, utetezi, ushirikiano na uchechemuzi wa kidigitali, Data takwimu kwaajili ya kuleta mabadiliko, Teknolojia, maadili, pamoja na ubunifu wa Teknolojia na maendeleo endelevu.
Nyingine ni pamoja na teknolojia katika ushirikiano na kuboresha uwazi, ujasiriamali na teknolojia kwa maendeleo endelevu, kuimarisha usalama mtandaoni, kuwawezesha wanawake na vijana kupitia teknolojia, kuweka wazi data na uwazi kwenye Utawala, pamoja na kutumia maarifa bandia yanayozingatia maadili Kwa manufaa ya jamii.
Kwa upande wake mshauri mwandamizi kutoka Shirika Norwegian Church, Anneth Torjusen amesema Mkutano huo pia kinalenga kujadili athari za tabia nchi na ni jinsi gani wananchi wanaweza kutumia teknolojia kwenye kilimo kukabiliana na tabia nchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa kitengo cha Sekta Binafsi kutoka Benki ya Stanbic Doreen Dominic, ambaye ni mfadili mkubwa wa wiki hii amesema Ushiriki wa taasisi yao katika CSO Week 2023 unadhamiriwa na hamu ya kuchochea ushirikiano na ubunifu.
‘’ Tunaelewa uwezo wa teknolojia katika kuendeleza maendeleo ya kijamii na kutatua changamoto muhimu zinazokabiliwa na nchi. Uwepo wetu kwenye tukio hili unalenga kuunganisha na mashirika yanayofikiri mbele, washirika watarajiwa, na wateja wa siku zijazo wanaoshiriki maono yetu. Kwa kumalizia, tunafurahi kuungana na mashirika ya kiraia, wapanga sera, na wataalamu wa teknolojia katika CSO Week 2023. Tunachukulia kuwa ushirikiano wetu unaweza kusaidia kutumia nguvu ya kubadilisha ya teknolojia na kuchochea athari chanya kwa jamii ya Tanzania, amesema.
Wiki ya AZAKI inaendeleza juhudi zake katika kuhakikisha ushirikishwaji bora na watendaji kutoka sekta mbalimbali hapa nchini.