Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla Elon Musk alisema Jumanne kampuni hiyo inatazamia kuwekeza nchini India haraka iwezekanavyo,kufuatia mkutano na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi huko New York.
“Modi anajali sana India kwa sababu anatusukuma kufanya uwekezaji mkubwa nchini India, ambalo ni jambo ambalo tunakusudia kufanya. Tunajaribu tu kujua wakati unaofaa, “Musk aliwaambia waandishi wa habari.
“Nina uhakika kwamba Tesla atakuwa India na atafanya hivyo haraka iwezekanavyo,” alisema, bila kutaja ratiba na kuwa ana mpango wa kuzuru India mwaka ujao.
Elon alikuwa amependekeza kuanzisha kiwanda cha kujenga magari ya umeme na pia alikuwa akiangalia utengenezaji wa betri za EV nchini.
“Wanaitazama India kama msingi wa uzalishaji na uvumbuzi,” waziri wa shirikisho Rajeev Chandrasekhar aliliambia shirika hilo mwezi Mei.
Mipango ya awali ya kampuni hiyo ya kufungua msingi nchini India ilisitishwa mwaka jana baada ya serikali ya India kusisitiza Tesla kutengeneza magari ndani ya nchi, huku kampuni ya kutengeneza magari ikisema inataka kusafirisha India kwanza ili iweze kupima mahitaji.
Bw Musk alisema kuwa anatumai pia kuleta huduma ya mtandao ya Starlink ya satelaiti, inayoendeshwa na kampuni yake ya SpaceX, nchini India.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, aliwasili New York Jumanne kwa ziara ya siku tatu ya serikali ambayo inaonekana kama hatua ya kubadilisha uhusiano wa nchi mbili kati ya India na Amerika.
Atakaribishwa kwa sherehe katika Ikulu ya White House siku ya Alhamisi kabla ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Rais Joe Biden.