Umoja wa mataifa jana uliadhimisha siku ya wakimbizi duniani, wakati ambapo wimbi la wakimbizi linaongezeka, na hivyo umoja huo unatoa wito kwa watu kuheshimu ujasiri na michango ya jamii za watu waliohamishwa kutoka makazi yao na vita, mateso, na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Siku ya wakimbizi duniani ya mwaka huu imeangazia hali mbaya ya wakimbizi milioni 35.4 na wanaotafuta hifadhi, juu ya mahitaji yao na haki za kisheria na usalama wao kote duniani.
Akizungumza kwenye hafla iliyofanyika katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma, kambi kubwa duniani, Filippo Grandi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ameipongeza serikali ya Kenya kwa mipango yake ya “kutekeleza sera bunifu na inayojumuisha watu wote.”
Wakati huo huo, katika ujumbe wake maalumu wa kuadhimisha siku hii ambayo ni Juni 20, Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amesema: Tunakabiliana na takwimu za kushangaza kwani “zaidi ya watu milioni 100 wanaoishi katika nchi zinazokumbwa na mizozo, mateso, njaa na machafuko ya mabadiliko ya tabianchi wamelazimika kuyahama makazi yao.
Wakati wamaadhimisho hayo taarifa zinasema zaidi ya watu milioni 2 na laki 5 wamelazimishwa kukimbia makazi yao kutokana na mzozo unaoendelea nchini Sudan, wakati huu ripoti za miili kutapakaa kwenye jimbo la Darfur Magharibi, zikizidisha wasiwasi.
Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, watu zaidi ya elfu 1 wameuawa katika mji wa Geneina peke yake, huku umoja wa Mataifa wenyewe ukisema watu elfu 2 wameuawa kiujumla tangu kuanza kwa mapigano mwezi April.
Aidha katika Siku ya Wakimbizi Duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, wakimbiizi wanahitaji na wanastahili kuungwa mkono na mshikamano sio kukutana na mipaka iliyofungwa na kurudi nyuma walikotoka.