Mataifa sitini, makampuni 400, wajumbe elfu moja wanakusanyika Jumatano hii Juni 21 na Alhamisi Juni 22 katika mji mkuu wa Uingereza, London, kwa ajili ya mkutano juu ya ujenzi wa Ukraine.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ambaye ameonekana kwenye video, amewahutubia wadau wa “kisiasa, kiuchumi na viongozi mbalimbali” waliokusanyika London, anaripoti mwandishi wetu huko London, Émeline Vin.
“Kwa kuijenga upya Ukraine, tutajenga upya uhuru. Rais wa Ukraine anatarajia, pamoja na mkutano huu, kushawishi makampuni na wawekezaji kurejea nchini. “Utulivu wa kimataifa unategemea utulivu wa Ukraine,” amekumbsha, akimaanisha kwa mfano kilimo na uzalishaji wa nishati.
Lengo lingine ni kuwahakikishia wawekezaji na kujiandaa kwa ajili ya kuimarika kwa uchumi wa nchi hii pindi vita vitakapomalizika. Rais wa Ukraine amezindua siku hizi mbili za majadiliano.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ilitangaza dhamana ya mkopo ya dola bilioni 3 kama sehemu ya mfuko mpya wa msaada wa kifedha kwa Ukraine ambao utasaidia kusaidia huduma za umma kama vile hospitali na shule.
“Swali kwetu leo ni nini tunaweza kufanya ili kuunga mkono hili – kuharakisha ahueni na kuisaidia Ukraine kudhihirisha uwezo wake. Ni lazima tulete ushirikiano wa serikali, taasisi za fedha za kimataifa, na viongozi wa biashara, sote hapa leo, ili kufanikisha hili,” Sunak alisema katika hotuba yake iliyotolewa kabla ya ufunguzi wa mkutano huo.
Ofisi ya Sunak pia ilisema kampuni 400 kutoka mataifa 38 zimeahidi kuunga mkono juhudi za ufufuaji na ujenzi mpya nchini Ukraine.
“Mahitaji ya ujenzi wa Ukraine ni – na yatakuwa – makubwa,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly alisema Jumanne. “Kupitia hatua zetu mpya leo, tunaimarisha mbinu ya vikwazo vya U.K., na kuthibitisha kwamba Uingereza iko tayari kutumia vikwazo ili kuhakikisha. Urusi inalipa kukarabati nchi ambayo imeshambulia kwa uzembe.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema Marekani itaendelea kuiunga mkono Ukraine, ikiwa ni pamoja na kutangaza Jumatano “mfuko mpya wa msaada wa Marekani.”
Blinken alisema mkutano huo ni onyesho la “uungwaji mkono wenye nguvu na wa kudumu kwa Ukraine, sio tu kijeshi lakini pia kiuchumi, na pia katika kila kitu tunachojaribu kufanya ili kujenga demokrasia yenye nguvu zaidi. Kwa hivyo, tunafurahi sana kuwa sehemu ya hili na ninafurahi sana kwamba Ukraine na marafiki zetu hapa wanaandaa mkutano huu.”