Muhammad Tezikuba Kisambira Balozi wa Uganda nchini Iran leo Jumatano amefanya mahojiano na shirika la habari la Iran Press huko Arak, makao makuu ya mkoa wa Kati hapa nchini. Katika mahojiano hayo, Balozi wa Uganda ameashiria ziara ya ujumbe wa kibiashara wa nchi yake katika mkoa huo na kuongeza kuwa: Wafanyabiashara wa Uganda katika ziara hiyo wanataka kuanzisha ushirikiano wa kibiashara, kuwekeza kwa pamoja, kuvutia uwekezaji na kushirikiana katika sekta ya utalii na mkoa wa Kati.
Balozi wa Uganda nchini Iran aidha ameeleza kuwa, ameshuhudia maendeleo makubwa ya kiteknolojia katika mkoa wa kati na kwamba kwa msingi huo wanaweza kuanzisha ushirikiano wa pande mbili katika nyanja za kibiashara na uwekezaji na kisha kupanua ushirikiano huo katika kiwango cha juu.
Balozi Muhammad Tezikuba Kisambira aidha ameeleza kuwa: Iwapo wakulima wa mkoa wa Kati hapa nchini watakuwa na hamu ya kulima zao la kahawa huko Uganda, serikali ya nchi hiyo inaweza kuwapatia bure ardhi yenye ukubwa wa kilomita mraba 40; ardhi ambayo itawapatia faida nyingine pia.
Balozi wa Uganda nchini Iran ameongeza kuwa, katika sekta ya mahindi pia Uganda inaweza kuiuzia Iran bidhaa hiyo moja kwa moja, na kwamba Uganda inaweza kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kisha kuiuzia mkoa wa Kati hapa nchini.
Balozi Muhammad Tezikuba Kisambira pia amesema kuwa mkoa wa Kati umepiga hatua nzuri katika sekta ya ujenzi, ujenzi wa nyumba na ujenzi wa barabara na kwamba pande mbili zinaweza kupanua ushirikiano wao wa pamoja. Balozi wa Uganda nchini Iran aidha ameutaja mkoa wa Kati wa Iran kuwa nyumba yake ya pili na kusema amemwalika Gavana wa mkoa huo kuitembelea Uganda; kwa sababu Kampala ina hamu ya kupanua ushirikiano wa nchi mbili katika nyanja za viwanda, kilimo na utamaduni.