Serikali ya Cameroon imesema haitamruhusu kuingia nchini humo balozi wa Ufaransa wa kutetea na kushajiisha vitendo vya ushoga, usagaji na watu kubadili jinsia zao (LGBT).
Balozi huyo wa Ufaransa, Jean-Marc Berthon ameratibiwa kwenda Cameroon kushiriki kongamano la kushajiisha vitendo hivyo vya ufuska, linalotazamiwa kufanyika baina ya Juni 27 na Julai Mosi katika mji mkuu Yaounde.
Kongamano hilo la kuwashawishi vijana wajihusishe na ubaradhuli linaandaliwa na taasisi moja ya Kifaransa. Hata hivyo maafisa wa serikali ya Cameroon wamesisitiza kuwa hawatamruhusu afisa huyo wa Ufaransa nchini kwao kwenda kupigia debe uchafu huo.
Aghalabu ya nchi za Afrika zinapinga vitendo vya ushoga na usagaji na watu kubadilisha jinsia zao. Baadhi ya nchi hizo zina sheria kali za kukabiliana na mienendo hiyo inayokwenda kinyume na maumbile ya mwanadamu.
Hivi karibuni, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alikataa wito wa nchi za Magharibi wa kufuta sheria dhidi ya ushoga iliyopasishwa na Bunge la nchi hiyo na kuidhinishwa na yeye mwenyewe.
Serikali ilituma notisi ya kidiplomasia kwa balozi wa Ufaransa nchini Cameroon kuashiria upinzani wake kwa ziara ya Berthon, kulingana na barua ya ndani iliyoonekana na shirika la habari la Reuters.
Notisi hiyo iliyotumwa Jumatatu, inaarifu ubalozi wa Ufaransa kwamba serikali inapinga shughuli zote zilizopangwa za Berthon, ikiwa ni pamoja na mkutano uliopendekezwa.
Nchi 22 tu kati ya 54 za Afrika zinaruhusu ushoga bali nchini Cameroon, mahusiano ya watu wa jinsia moja yanaweza kusababisha kifungo cha hadi miaka mitano jela.
Unyanyasaji dhidi ya jumuiya ya LGBT+ nchini humo unaongezeka, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kikatili na kukamatwa kiholela, kulingana na Human Rights Watch.
Safari iliyopangwa ya Berthon kwenda Cameroon inakuja wiki kadhaa baada ya Uganda kupitisha mojawapo ya miswada mikali zaidi duniani dhidi ya LGBTQ, ikiwa ni pamoja na utoaji wa vifungo vya muda mrefu na hukumu ya kifo.