Mbunge wa Jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani ameiomba serikali kuendelea kupunguza kodi zinazowabana wanunuzi wa tumbaku nchini ili wakulima wa zao hilo waendelee kupata faida kubwa.
Mheshimiwa Cherehani ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 ambapo pia ameeleza kilio cha wakulima wa pamba nchini wanaouza kwa bei ya chini na kuiomba serikali kuwepo kwa mfuko wa pembejeo na kinga ya mazao hususani mazao ya kimkakati pindi bei ya masoko inapotikisika.
“Leo hii wakulima wa pamba wametumia gharama kubwa kuzalisha zao lao na kulima Pamba nyingi baada ya kupelekewa mbegu kwa bei ya ruzuku, tunaomba kama mtikisiko wa bei unapotokea kuwe na maadalizi ili kuweka kinga kwa mazao ya kimkakati”.
“Wakulima wa Tumbaku wanahitaji kulipwa fedha zao kwa dola, Waziri wa Fedha amesema Serikali ina akiba ya dola kwahiyo tunaomba wakulima wetu waendelee kulipwa kwa dola kama utaratibu tuliojiwekea kwenye halmashauri ya tumbaku”.